NEC yatoa maamuzi kuhusu rufaa ya uchaguzi mdogo

Mgombea udiwani wa chama cha Wananchi (CUF), Mdohoma Bashiru Ismaili amerejeshwa kwa mara nyingine katika kinyang'anyiro cha kugombea nafasi ya udiwani, wa kata ya Kibutuka katika halmashauri ya wilaya ya Liwale mkoani Lindi, baada ya rufaa yake kutolewa maamuzi bila ya kupingwa.



Hayo yamebainishwa na taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Hamis Mkunga leo Septemba 30, 2018 na kusema kuwa maamuzi hayo yamefanyika kwa kufuatia kikao kilichoketi leo na kukubaliana na maelezo yaliyotolewa na mkataji rufaa huyo ambaye alitaka kurejeshwa kuwa mgombea udiwani katika Kata ya Kibutuka kupitia chama hicho.
"Tume katika kikao chake cha tarehe 30 Septemba 2018, imekubaliana na maelezo ya mrufani na kuelekeza arejeshwe kuendelea kuwa mgombea Udiwani katika Kata ya Kibutuka, Halmashauri ya wilaya ya Liwale kwa kuwa imejiridhisha kwamba mrufani wakati wa kujaza fomu yake ya uteuzi Na. 8C alianza na jina la mwisho likifuatiwa na majina mengine kwa kuwa ndilo alilotaka lianze kuandikwa kwenye karatasi ya kupigia kura.......
Kwa mujibu wa maelekezo ya Tume kuhusu ujazaji wa fomu Na. 8 C ya uteuzi katika kipengele namba (2), yanatoa uhuru kwa mgombea kuanza na jina ambalo angetaka liandikwe kwa herufi kubwa kwenye  karatasi ya kupigia kura", amesema Mkunga.
Mbali na hilo, NEC imevitaka vyama vya siasa na wagombea wanaoshiriki uchaguzi mdogo wa Ubunge katika jimbo la Liwale na Udiwani katika Kata mbalimbali za Tanzania Bara, utakaofanyika Oktoba 13, 2018, wazingatia sheria na maadili ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2015, wakati wote wa kampeni na hata siku ya uchaguzi.
Uchaguzi mdogo wa marudio katika jimbo la Liwale na kwenye Kata 37 za Tanzania Bara, unafanyika baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo (CUF), Zuberi Kuchauka.
Hata hivyo, CHADEMA kupitia kwa Mwenyekiti wake Taifa, Freeman Mbowe, alitangaza kususia uchaguzi huo na wa kata 37 na chaguzi zinginezo zinazokuja.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HADITHI:MWALIMU MAGDALENA sehemu ya 1

Hadithi: Mwalimu Magdalena sehemu ya 5

Hadithi: Mwalimu Magdalena sehemu ya 4