Sahau tena kusikia mchezaji anauguza jeraha

KUKUA kwa teknolojia kunaendelea kuleta mageuzi makubwa duniani, ikiwamo sekta ya michezo ambayo pia imekuwa ikiguswa na mapinduzi haya ya kidigitali.
Kwani tunashuhudia matukio mengi ya kimichezo kwa sasa yakirushwa kisasa zaidi tofauti na miaka kadhaa iliyopita, jambo ambalo linachagizwa na kuwapo kwa wabunifu mbalimbali ambao wamekuwa wakiumiza vichwa kwa ajili ya kuona michezo ikibadilika na kuendeshwa kisasa zaidi kutokana na mabadiliko ya teknolojia.
Hivi sasa teknolojia hiyo imebadilisha ubora na mwonekano wa matangazo ya michezo mbalimbali duniani kutoka viwanjani, jambo ambalo limesukuma hata klabu kujikuta vikiwekeza kwenye wachezaji mahiri ambao watawasaidia kusukuma bidhaa zao katika masoko makubwa duniani na kuingiza fedha nyingi hasa kupitia teknolojia.
Habari ya kuvutia leo kwenye ulimwengu huu wa teknolojia michezoni ambayo naamini hata wewe ungetamani kuisikia, ni namna ambavyo mchezaji atakavyokuwa anatibiwa kwa kutumia teknolojia pindi anapopata majeraha akiwa uwanjani.
Hii ina maana kwamba vifaa vya kielektroniki ndivyo vitakavyotumika katika kuhakikisha kuwa vinatoa majibu kwenye benchi la madaktari wa timu husika juu ya tatizo lililomkuta mchezaji kabla hata ya kutolewa nje ya uwanja.
Taarifa zinasema kuwa madaktari watakuwa wakipata taarifa na video za moja kwa moja juu ya tatizo lililomfika mchezaji akiwa uwanjani na namna gani ya kulikabili kupitia mfumo maalumu utaounganishwa moja kwa moja kwenye televisheni uwanjani.
Uamuzi huu umetangazwa na Bodi ya Chama cha Mpira wa Miguu cha Kimataifa (IFAB) kwenye mkutano wake wa mwaka.
Bodi hiyo imesema kuwa kupitisha maamuzi hayo ni kwa jili ya kutaka kuwasaidia wachezaji ikiwamo kupatiwa matibabu ya haraka pindi wanapopata tatizo ili kulinda afya zao, jambo litakalowaepusha kukaa nje ya uwanja kwa kipindi kirefu.
Baadhi ya vifaa vya teknolojia vitakavyohusika ni pamoja na tableti, kompyuta na vifaa vingine muhimu ambavyo vitasaidia matibabu ya haraka kwa mchezaji atakayekumbwa na tatizo akiwa uwanjani.
“Tunaelewa na kuamini kutoka kwa wataalamu kuwa iwapo unakuwa na mifumo ya kisasa ya kusaidia kugundua tatizo la mchezaji, inakuwa ni rahisi zaidi kumtibu kuliko kuanza kumfanyia vipimo ili kubaini tatizo kwani wakati mwingine tatizo linaweza lisionekane papohapo.
“Hivyo tumepata mifano ya kutosha namna ambavyo mfumo huu utakuwa rafiki kwa wachezaji pindi madaktari wanapotumia majibu ya teknolojia hii kuweza kubaini tatizo, hii inamsaidia mchezaji kuwa na uhakika wa kuendelea kucheza na si kukosa baadhi ya michezo kwani matibabu yake ni ya haraka kulingana na teknolojia, tuna imani kuwa wapenda michezo wote duniani wataipokea vizuri taarifa hii,” anasema Katibu wa IFAB, Lukas Brud.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HADITHI:MWALIMU MAGDALENA sehemu ya 1

Hadithi: Mwalimu Magdalena sehemu ya 5

Hadithi: Mwalimu Magdalena sehemu ya 4