Usikose APPS hizi kama unapenda michezo
NA FARAJA MASINDE,
KATIKA miaka hii ya karibuni teknolojia inaendelea kuchukua nafasi kubwa zaidi duniani katika kusukuma michezo na hili ndilo limekuwa moja ya maeneo yanayoongeza wafuasi wengi zaidi kwenye michezo mbalimbali.
Ni kweli kuwa mapinduzi haya ya teknolojia yamefanya mambo mengi kwa sasa katika upande wa michezo kuendeshwa kisasa zaidi.
Asilimia kubwa ya michezo mingi imekuwa ikionekana moja kwa moja kupitia televisheni na hata matangazo ya moja kwa moja kupitia redio, achilia mbali vipande vifupi vya video mbavyo vimekuwa vikisambazwa katika kuonyesha matukio muhimu ya mchezo husika.
Leo hii tunashuhudia kuwa kupitia teknolojia mtu unao uwezo wa kupata matokeo na taarifa za papo kwa papo kupitia ‘application’ mbalimbali.
Ni wazi kuwa eneo hili la teknolojia linazidi kipeleke mbali zaidi tasnia ya michezo na hata kuwavutia wengine ambao hawakuwa na lengo la kujihusisha na michezo hiyo.
Tambua kuwa ni kukua kwa teknolojia huko ndiko kumefanya hata mtoto wa miaka mitano leo anamtambua mtu kama Lionel Messi, Cristino Ronaldo, Paul Pogba, Serena William, LeBrown James, Usain Bolt, Tiger Wood na wengine wengi.
Ni mapinduzi haya ya teknolojia ndiyo yanayoendelea kuwa tija na faraja kubwa kwa wabunifu mbalimbali, kwani kwa kipindi cha miaka michache iliyopita na hivi leo tunashuhudia kuwapo kwa Apps nyingi za michezo ambazo zinapatikana kupitia programu endeshaji mbalimbali, zikiwamo Android na iOS.
Natambua kuwa zipo baadhi unazozitambua na nyingine ambazo kwa kujua au kwa kutokujua zimekuwa zikikupita kushoto na kusalia kuona wenzio wakifurahia ulimwengu huu wa teknolojia kwenye michezo.
Hizi ni baadhi ya Apps, kama wewe unapenda michezo na muda mwingine unakosa muda wa kujongea kwenye televisheni kutazama au kufuatilia moja kwa moja kutokana na changamoto za kusaka mkate wa kila siku.
Na wakati mwingine kutumia muda wako mwingi Gym kwa ajili ya siku moja kuja kufikia ndoto yako ya kuwa kama Mbwana Samatta kama siyo Neymar Junior basi Apps hizi zitakufaa.
Thuuz Sports
Hii ni Apps ambayo kadri siku zinazvyozidi kusonga ndivyo pia inavyoendelea kujiongezea umaarufu, programu hii imetengenezwa na Thuuz Sports, ambapo kwa siku za hivi karibuni imeendelea kuwa maarufu zaidi duniani.
Jambo la ziada kwenye programu hii ni kuwa inakupa uhuru wa kuangalia timu zako unazopenda upokee matokeo yake tu na kama kuna baadhi ya timu huna habari nazo basi apps hii pia haitakuletea habari za timu husika.
Feedly
Apps hii inakupa nafasi ya kutambua bei za bidhaa mbalimbali zinazohusu michezo kutoka sehemu mbalimbali ambapo kwa sasa waasisi wa Apps hii wanaangalia namna ambavyo mtu anaweza kutumia kununua vifaa hivyo moja kwa moja kwa maana ya ONLINE kutoka kwenye maduka mbalimbali.
CBS Sports
Hii ni Apps ambayo imekuwa ikichukua programu za zamani za mazoezi na kuzileta kwenye usasa, ikiwamo pia kukusaidia namna gani wewe unavyoweza kufanya mazoezi.
Programu hii imeonekana kupendwa zaidi, kwani kwa kiwango kikubwa imeonekana kuwasaidia watu wengi, kwani mbali na programu za mazoezi, pia imekuwa ikiwakumbusha watembeleaji wake matukio na rekodi mbalimbali zilizowahi kuwekwa miaka ya nyuma kuhusu michezo.
NFL Mobile
Programu hii yenyewe imejikita zaidi katika kutoa bure video za matukio ya michezo mbalimbali kwa watumiaji wote wa Apps hii.
Hivyo, Apps hii imekuwa ikijikita zaidi kwenye eneo la ligi ya kikapu ya Marekani ambapo imekuwa ikitoa msaada mkubwa kwa wale wote wanaopenda kufuatia mchezo wa kikapu wa nchi hiyo, zikiwamo pia taarifa za wachezaji hao wanaowapenda.
Team Stream
Apps hii linapokuja suala la wastani wa taarifa za michezo basi imekuwa ni namba moja, kwani imekuwa ikileta pamoja safu na makala mbalimbali, ikihusisha chambuzi mbalimbali za masuala ya soka ambazo huwekwa kwenye Apps hii kwa kuzingatia kuwa hazina maudhui ya matusi.
Ili kuwasaidia wafuasi na wafuatiliaji wa makala mbalimbali za michezo, hii ndiyo imekuwa sababu kubwa kwa waandishi wa safu mbalimbali za michezo duniani kuwa maarufu na kutambulika zaidi, kwani kazi zao nyingi zimekuwa zikipakiwa kwenye app hii pamoja na kupewa kipaumbele zaidi.
TheScore & ESPN
Hizi ndizo Apps kubwa zaidi na maarufu ambazo zinafanya vyema kwenye eneo la michezo, hasa linapokuja suala linalohusu habari na matokeo mbalimbali ya michezo yote.
Umaarufu wa Apps hizi unachagizwa na kutoa taarifa kwa wakati na zenye ukweli ikilinganishwa na Applications nyingine.
Apps hizi zinatajwa kuwa ndizo Apps zenye mamilioni ya wafuasi wengi zaidi duniani, hii ikichagizwa na umakini wao katika kutoa taarifa kulingana na matukio mbalimbali, hata hivyo, utendaji bora wa waendeshaji wa Apps hizi ndiyo unatajwa kama chanzo cha mafanikio yake.
Hivyo ili kuwa na Apps hizi, kazi ni kwako kuhakikisha kuwa unapakua unayoona inakufaa katika maisha yako.
0653045474
Maoni
Chapisha Maoni