Mastaa duniani wanavyowekeza kwenye teknolojia
NA FARAJA MASINDE,
JUKUMU langu ni kuhakikisha maktaba ya ubongo wako inapata madini yote kuhusu teknolojia michezoni.
Huwezi kubisha nikikwambia kuwa, eneo hili la teknolojia limekuwa na faida kubwa iwapo litatumika vema, kwani hata wanamichezo wamenusa fursa hii na kuona kumbe wanaweza kutengeneza mkwanja mrefu kwa kufanya uwekezaji kwenye sekta hii.
Ni kweli kwamba tunashuhudia kama siyo kusikia mara kwa mara jarida maarufu duniani lenye jukumu la kutusaidia kuchungulia akaunti za mastaa na watu maarufu la Forbes likitupa orodha ya vitita vya fedha wanavyomiliki wachezaji wakubwa wa dunia kama, Cristano Ronaldo na wengine.
Sports teknolojia kama moja ya safu bora kuwahi kutokea inayounganisha michezo na teknolojia, inayo orodha ya wachezaji walioamua kukata shauri na kwenda kuwekeza kwenye eneo hili hivyo kujikuta wakitengeneza fedha nyingi bila kelele.
Na hapa ndipo inapokuja tofauti kubwa kati ya midfield Hussein Masha (Simba) na Steven Gerald (Liverpool) licha ya ukweli kwamba, wote waliwahi kung’ara kutokana na kuuchezea mpira ipasavyo, lakini tukija kwenye mafanikio Gerald ana mafanikio makubwa hasa ya kifedha.
Majina kama Ronaldo, Michael Owen na Louis Saha haya ni baadhi ya majina ya wachezaji wachache walioamua kutengeneza fedha ndefu kupitia kuwekeza kwenye teknolojia.
Louis Saha
Uwekezaji uliofanywa na Louis Saha ambaye ni mchezaji mstaafu wa Timu ya Taifa ya Ufaransa, aliyewahi kukipiga kwenye timu mbalimbali zinazoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ni mkubwa.
Saha anamiliki teknolojia yake ya ‘Set Up’ ambayo ameipa jina la ‘Axis Stars’. Application hii imetengenezwa kama jukwaa la mtandaoni (Online Platform Designed) ikiwa na lengo moja tu, kuwasaidia wachezaji chipukizi kupata mawakala na wadhamini.
Saha anasema kuwa, binafsi anaamini kwa wachezaji kuwa na timu ya kuchezea, Wakala na mdhamini kwenye sehemu moja inaleta matokeo ya uwazi na kupunguza mianya ya ‘upigaji’ rushwa.
“Hakuna mtu yeyote anaweza kuvuruga mfumo huu, licha tu kwamba umewasaidia wengi, lakini lengo langu ni kuona mfumo huu ukisalia kuwa bora zaidi na faraja kwa kizazi cha sasa na kijacho ili kuona rekodi mbalimbali za watangulizi wao,” anasisitiza Saha.
Andres Iniesta
Kama umewahi kufuatilia michezo ya FC Barcelona utakubaliana na mimi kuwa, Iniesta amekuwa ni mchezaji wa kutumainiwa mno kwenye klabu hiyo kwa kipindi cha miaka 10.
Iniesta hajakaa mbali na teknolojia kwani amewekeza kwenye ‘Firstvision’, iliyoundwa kwa mfumo wa camera na video. Kazi yake kubwa ni kuchukua matukio yote yanayofanywa na mchezaji husika kuanzia viatu anavyovaa na matukio yote ya kimichezo yanayomhusu.
Mara baada ya kukamilisha kuchukua matukio hayo, kampuni hiyo hutundika video hizo kwenye mtandao wake pamoja na ule wa YouTube, hapo unaweza kuyaona matukio yote ya mchezaji kuanzia namna anavyopiga mpira na hata kutembea.
Cristiano Ronaldo
Mshambuliaji huyu wa Real Madrid ni moja ya majina ambayo yamekuwa mstari wa mbele katika kucheza na mashabiki kupata mkwanja kupitia uzito wa jina lake.
Ronaldo ambaye amekuwa na historia kubwa kama siyo ya kipekee kwenye soka la kizazi hiki, amewekeza kiasi kikubwa cha fedha kwenye teknolojia ya Mobbito.
Mobbito ni application ‘App’ ya Kireno ambayo inatoa uhuru watumiaji wake kutengeneza timu na kisha kuzawadiwa na wafanyabiashara wa ndani nchini humo.
Licha ya kwamba hajaianzisha Ronaldo, lakini ameweka App hiyo inayoelezwa kuwa na nguvu kubwa katika kuona kuwa inafanikiwa, hivyo amekuwa ni sehemu ya mafanikio ya App hiyo.
Michael Owen
Najua kama unalikumbuka hili jina, kwani ni kati ya yale yaliyowahi kusumbua kwenye ulimwengu huu wa soka, ni kweli kwamba ni mchezaji mstaafu wa Timu ya Taifa ya Uingereza, licha ya kwamba amestaafu soka lakini amerudi kivingine, safari hii yuko nyuma ya teknolojia.
Owen ameamua kuanzisha jukwaa lake la mtandao wa kijamii ambalo amelipa Jina la Sportlobster, tovuti hii inahusisha michezo tofauti takribani 32 na ilianzishwa maalum kwa ajili ya mashabiki wa michezo kutembelea na kujua taarifa, matokeo, video mbalimbali kwenye moja ya michezo iliyoko humo.
Mashabiki pia kutoka kote ulimwenguni wanaweza kuchati, kupata fununu na hata kutembelea tovuti nyingine. Tovuti hiyo ilizinduliwa mwaka 2013, inapatikana mtandaoni na kwenye Apps za Androids na iOS ambapo inazaidi ya watembeleaji milioni 1.4, akiwamo Cristian Ronaldo ambaye alihusishwa makusudi kwa ajili ya kuipa soko tovuti hiyo.
Maoni
Chapisha Maoni