Nigeria yafanya maandamano ya kumuunga mkono Sheikh Zakzaky
Wananchi wa Nigeria wamefanya maandamano kulalamikia kuendelea
kuwekwa korokoroni kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo.
Sheikh Ibrahim Zakzaky anaendelea kushikiliwa mahali
pasipojulikana huko Nigeria bila ya kushtakiwa licha ya kupita zaidi ya
miezi mitatu sasa tangu atiwe mbaroni. Wakazi wa mji wa Zaria katika
jimbo la Kaduna kaskazini mwa Nigeria jana waliandamana kulalamikia
kuendelea kuzuiliwa korokoroni Sheikh Ibrahim Zakzaky Kiongozi wa
Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, huku wakiwa wamebeba mabango na kupiga
nara zinazosema "Muachieni huru Sheikh Zakzaky."
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, maandamano hayo yamefanyika huku Harakati
ya Kiislamu ya Nigeria ikikanusha madai kuwa wanachama wa harakati hiyo
wiki iliyopita walimteka nyara kanali mmoja wa jeshi na kumuua.
Vikosi vya jeshi la Nigeria mwezi Disemba mwaka jana viliishambulia
nyumba ya Sheikh Ibrahim Zakzaky katika mji wa Zaria jimboni Kaduna na
husseiniya kadhaa nchini humo, na kisha kumjeruhi na kumtia nguvuni
kiongozi huyo wa kidini na kuua pia idadi kubwa ya Waislamu wa mji huo.
Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imetangaza kuwa watu zaidi ya 12
waliotiwa mbaroni kwenye mashambulizi ya jeshi la Nigeria, hadi sasa
hawajapata huduma za kitiba licha ya kujeruhiwa vikali katika
mashambulizi hayo. Wiki iliyopita pia wananchi wa Nigeria walifanya
maandamano katika miji mbalimbali ya nchi hiyo na kulaani kuendelea
kushikiliwa Sheikh Ibrahim Zakzaky Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya
nchi hiyo. Wafanya maandamano katika miji ya Lafia, Katsina, Gombe na
Kaduna wametaka kuachiwa huru haraka iwezekanavyo Sheikh Zakzaky na
Waislamu wengine ambao wanashikiliwa katika korokoro za jeshi la
Nigeria. Baada ya kupita miezi kadhaa tangu Sheikh Zakzaky atiwe nguvuni
na jeshi la Nigeria, hatimaye shakhsia mmoja aliye karibu na Kiongozi
huyo wa Harakati ya Kiislamu wiki kadhaa zilizopita alifanikiwa kuonana
na Sheikh Zakzaky na mkewe.
Mtu huyo aliye karibu na Sheikh Zakzaky alisema kuwa, hali ya mke wa
kiongozi huyo imeboreka japokuwa wameshindwa kutoa mwilini mwake risasi
moja kwa kuhofia kuwa huenda likamfanya kuwa kilema.
Shakhsiya huyo aliye karibu na Sheikh Zakzaky ameongeza kusema kuwa,
Sheikh Ibrahim Zakzaky naye pia anaendelea kupata matibabu, ingawa kwa
bahati mbaya jicho lake moja limepoteza kabisa uwezo wa kuona na jingine
pia kupoteza uwezo mkubwa wa kuona.
Duru hiyo imeendelea kubainisha kuwa, Sheikh Zakzaky ameanza
kutembea kwa taabu hivi karibuni tu kutokana na kujeruhiwa vikali na
vikosi vya Nigeria, lakini pamoja na nayo, yeye na mkewe wanaonekana
kuwa na motisha ya hali ya juu.
Baada ya kufanyika ziara hiyo, viongozi wa Nigeria waliizuia timu ya
uchunguzi ya Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo kuonana na kiongozi wao,
na kwa msingi huo harakati hiyo nayo ikaamua kutohudhuria mahakamani.
Timu ya kisheria ya Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imeitaja hatua ya
kunyimwa kibali cha kuonana na Sheikh Zakzaky ambaye anashikiliwa
katika seli za jeshi la nchi hiyo kuwa ni kitendo kisicho cha kiakhlaqi
na kilicho kinyume na maadili.
Katika upande mwingine, Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Kiislamu ya
Uingereza wiki iliyopita ilitoa taarifa na kueleza kuwa, imewasilisha
katika mahakama ya ICC ya The Hague faili la kesi ya kushambuliwa
nyumba ya Sheikh Ibrahim Zakzaky na vikosi vya usalama vya Nigeria.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, uhalifu uliofanywa na jeshi la Nigeria
katika kipindi cha tarehe 12 hadi 14 Disemba katika mji wa Zaria dhidi
ya Waisalmu ni jinai dhidi ya binadamu na kuna udharura wa kutolewa amri
ya uchunguzi wa mahakama ya ICC kuhusu uhalifu huo. Kamisheni ya Haki
za Binadamu ya Kiislamu ya Uingereza imesisitiza kuwa ushahidi uliopo
unaonyesha kuwa, shambulio hilo dhidi ya Kiongozi wa Harakati ya
Kiislamu ya Nigeria ambalo limeweza kuwavutia wafuasi wengi kaskazini
mwa nchi hiyo, lilikuwa ni shambulizi lililopangwa.
Masoud Shajare Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Kiislamu ya
Uingereza amesema kuwa taathira kubwa za jinai hizo na kushindwa
serikali kufuatilia kisheria kadhia hiyo, yote hayo yanatoa udharura wa
kufuatiliwa mwenendo wa kesi hiyo katika Mahakama ya Kimataifa.
Iran swahili
Maoni
Chapisha Maoni