Mayanja: Azam, Yanga wasijidanganye
BAADA ya Yanga, Azam FC kutinga nusu fainali ya Kombe
la FA, Kocha wa Simba, Jackson Mayanja amesema hana presha yoyote juu ya timu atakayokutana
nayo katika hatua zinazofuata za michuano hiyo kati ya wapinzani wake hao ambao
wamekuwa wakijitanganya wakijiona wao ni kila kitu kwenye soka la Tanzania.
Kocha wa Simba, Jackson Mayanja |
Yanga na Azam juzi zilifanikiwa kutinga nusu fainali
ya Kombe la FA baada ya kushinda michezo yao ya robo fainali ambapo
Wanajangwani waliwachapa Ndanda FC mabao 2-1, huku Wanalambalamba wakiipiga Tanzania
Prison mabao 3-1 kwenye viwanja Taifa na Azam Complex, Dar es Salaam.
Timu nyingine iliyotinga nusu fainali ni Mwadui,
huku Simba ikisubiriwa kuungana na wenzake hao iwapo itaitoa Coastal Union wiki
ijayo.
Akizungumza na BINGWA jijini jana, Mayanja alisema
anachokiangalia kwa sasa ni kuhakikisha timu yake inafanya vizuri ili waweze
kutinga nusu fainali.
Alisema wakishinda mchezo wao huo dhidi ya Coastal, hakuna
timu ambayo ataihofia mbele yao, iwe ni Azam au Yanga.
Azam Fc |
“Ninachoangalia ni kuhitaji ushindi katika mchezo
wetu na Coastal, nikitinga hatua ya nusu fainali, sitahofia Azam wala Yanga,
kwani nina imani na kikosi changu kufanya vizuri katika michuano hii pamoja na ligi,”
alisema.
Mayanja alisema mara nyingi anakuwa na hofu na
wachezaji wake na si mpinzani wake, kwani vijana wake wakishindwa kufuata
maelekezo watamuangusha.
“Kikubwa nafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza
katika mechi zilizopita ili kujenga kikosi imara, kwa kuwakumbusha vijana wangu
kwamba tunahitaji kushinda katika mapambano yanayotukabili,” alisema.
Mayanja alisema kikosi chake kipo vizuri na kwa
wachezaji ambao walikuwepo katika kikosi cha timu za taifa, ambao hawajajiunga
na wenzao ni Hamis Kiiza, Jjuuko Murushid na Mwinyi Kazimoto.
“Kiiza na Jjuuko watajiunga mapema, lakini Kazimoto
anaumwa na anatakiwa kukaa nje kwa muda wa wiki mmoja, kama hajapona hadi muda
huu hataathiri timu na kuhakikisha tunamtafuta wa kuiziba nafasi yake,” alisema
Mayanja.
Bingwa
Maoni
Chapisha Maoni