Amnesty: Uturuki imewatimua wakimbizi
Shirika la kutetea haki za binadamu duniani, Amnesty International
linadai kuwa na ushahidi unaoonyesha kwamba Uturuki imewarudisha
nyumbani wakimbizi wa Syria kinyume cha sheria.
Shirika hilo limesema maafisa wa Uturuki wamekuwa wanawakamata na
kuwarudisha wakimbizi wa Syria katika makundi ya watu mia mia, wanaume,
wanawake na watoto kila siku, tangu katikati ya mwezi wa Januari.
Wengi miongoni mwa wakimbizi hao walikuwa wale ambao hawakusajiliwa
rasmi. Hata hivyo asasi ya Amnesty International imedai kuorodhesha
mikasa ya wakimbizi waliofukuzwa ambao walikuwa wamesajiliwa.
Watu hao walirudishwa nchini Syria kwa sababu hawakuwa na hati zao za usajili wakati walipokamatwa.
Wakimbizi wauliwa kwa kupigwa risasi
Wakati huo huo shirika la Syria la kutetea haki za binadamu lenye makao
yake mjini London limesema limepata ushahidi unaonyesha jinsi wakimbizi
16 walivyopigwa risasi na kufa ,wakati walipokuwa wanajaribu kuuvuka
mpaka wa Syria ili kuingia Uturuki.Lakini shirika hilo linaamini idadi
ya waliouawa inaweza kuwa kubwa zaidi.
Hatua iliyochukuliwa na Uturuki inadhihirisha hatari kubwa inayowakabili
wakimbizi wanaorudishwa kutoka Ulaya, kutokana na mkataba uliofikiwa
baina ya Uturuki na Umoja wa Ulaya unaotarajiwa kuanza kutekelezwa wiki
ijao.
Uturuki ilikubaliana na Umoja wa Ulaya juu ya kuwarudisha wakimbizi
wanaoingia Ugiriki, kinyume cha sheria kuanzia mwezi huu. Na kwa
kuyatekeleza makubaliano hayo Uturuki itapatiwa msaada wa fedha . Pia
mchakato wa kuwaruhusu raia wa Uturuki kuingia katika nchi za Umoja wa
Ulaya bila ya visa utaharakishwa.
Aidha mazungumzo juu ya Uturuki kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya yataharakishwa kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa.
Hata hivyo uhalali wa mkataba huo unategemea, iwapo Uturuki ni nchi
salama kwa watu wanaoomba hifadhi ya ukimbizi, lakini katika ripoti yake
shirika la kutetea haki za binadamu,Amnesty International limesema ni
wazi kwamba nchi hiyo si salama kwa wanaoomba hifadhi ya ukimbizi.
Shirika la Amnesty International limesema kurudishwa kwa nguvu nchini
Syria kwa watoto watatu bila ya wazazi wao pamoja na mwanamke mjamzito
ni miongoni mwa mikasa lililoorodhesha.
Hata hivyo wizara ya mambo ya nje ya Uturuki imekanusha madai kwamba imewarudisha kwao wakimbizi wa Syria bila ya hiyari zao.
Wizara hiyo imesema Uturuki imekuwa inaitekeleza sera ya milango wazi
kwa wakimbizi wa Syria kwa muda wa miaka mitano iliyopita na pia
imeizingatia kanuni ya kutowarudisha wakimbizi katika nchi ambako
wanaweza kuwamo katika hatari ya kuandamwa.
Ujerumani kuchukua wakimbizi
Wakati huo huo Ujerumani imesema itawachukua wakimbizi wa kwanza wa
Syria kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya Uturuki na Umoja
wa Ulaya.
Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya Ujerumani amearifu kuwa idadi
kubwa ya wakimbizi hao wanaotarajiwa kuanza kuwasili Jumatatu ijayo ni
familia zenye watoto.
Kwa mujibu wa utaratibu uliokubaliwa pamoja na Umoja wa Ulaya kwa kila
mkimbizi wa Syria ataekepewa hifadhi kihalali barani Ulaya,mwengine
atachukuliwa na Uturuki kutoka Ugiriki.
Lakini shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International
limesema kurudishwa kwa nguvu kwa wakimbizi wa Syria kunaonyesha kasoro
zilizomo katika makubaliano yaliyofikiwa baina ya Uturuki na Umoja wa
Ulaya.
DW
Maoni
Chapisha Maoni