Miaka 30 jela kwa kuoa binti wa miaka minane
MKAZI wa Kijiji cha Nyaburundu wilayani Bunda,
Changwe Changige (54), amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumuoa
na kumbaka binti mwenye umri wa miaka minane.
Pia baba mzazi wa binti huyo ambaye ni mkazi wa
kijiji hicho, Kakwa Runguya (53), naye amehukumiwa miaka mitano jela kwa kosa
la udhalilishaji kwa kumuoza binti yake kwa mwanamume huyo.
Mahakama ya Wilaya ya Bunda ilidai kuwa baba huyo amehukumiwa
kutumikia kifungo hicho kwa kumuoza binti yake na kumnyima fursa ya kusoma.
Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Hamza Mdogwa, alidai kuwa
washtakiwa wote wawili walitenda makosa hayo Januari Mosi, mwaka jana saa 10
jioni katika kijiji hicho.
Mdogwa alidai kuwa washtakiwa wote wawili walishtakiwa
kwa kosa la kwanza ambalo ni kula njama na kumuoza binti huyo huku Changwe
aliyemuoa na kumbaka binti huyo alishtakiwa kwa kosa la pili la ubakaji na
Kakwa alishtakiwa kwa kosa lingine la udhalilishaji.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu wa mahakama hiyo, Hamad
Kasonso, alisema katika kosa la kwanza la kula njama na kumuoza binti huyo washtakiwa
wote kwa pamoja watatumikia kifungo cha mwaka mmoja jela kila mmoja.
Kasonso alisema katika kosa la pili, Changwe atatumikia
kifungo cha miaka 30 na katika kosa la tatu ambalo ni la udhalilishaji, Kakwa
atatumikia kifungo cha miaka mitano jela.
Kabla ya hukumu hiyo kutolewa, washtakiwa wote
walijitetea wapunguziwe adhabu ingawaje utetezi huo ulitupiliwa mbali na
mahakama hiyo baada ya Hakimu Kasonso kudai kuwa adhabu hiyo itakuwa fundisho
kwao na kwa watu wengine wenye nia au tabia ya kuoza ama kuoa na kubaka watoto
wadogo.
Katika kesi nyingine, mkazi wa Kijiji cha Mariwanda
wilayani Bunda, Athuman Jeki (45), amefikishwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu
Mkazi Mfawidhi Gadiel Maliki, kwa kosa la kumbaka binti yake mwenye umri wa
miaka tisa.
Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Masoud Mohamed,
aliiambia mahakama hiyo kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Novemba 27,
mwaka huu saa nne asubuhi katika Kijiji cha Mariwanda.
Mohamed aliiambia mahakama hiyo kuwa siku ya tukio
mshtakiwa alimbaka binti yake nyumbani kwake, wakati mke wake akiwa hayupo na
kumsababishia maumivu makali na kusababisha kulazwa katika Hospitali ya Wilaya
ya Bunda.
Mshtakiwa huyo alikana shtaka lake na kupelekwa
mahabusu hadi Desemba 17, mwaka huu kesi yake itakapotajwa tena mahakamani
hapo.-Mtanzania
Maoni
Chapisha Maoni