Vigogo Yanga wampandia Maguli
YANGA wanatarajia kukamilisha usajili wa dirisha dogo la Ligi Kuu Tanzania
Bara na michuano ya kimataifa baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la
Chalenji inayoendelea mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Viongozi wa Yanga na benchi la ufundi la timu hiyo kwa sasa wako makini
sana kuhakikisha wanapata wachezaji makini wa kuongeza nguvu kwenye kikosi chao
ili kuhakikisha wanafanya maajabu katika michuano inayoendelea hasa ile ya kimataifa
itakayoanza hapo mwakani.
Maguli na Canavaro
Kutokana na hali hiyo zoezi la usajili kwenye klabu hiyo ya Jangwani
limekuwa likifanyika kwa umakini mno, hasa katika kipindi hiki cha dirisha dogo
na ndiyo maana hadi sasa bado hawajaweka wazi mipango yao ya usajili.
Chanzo cha kuaminika kimeliambia BINGWA kwamba tayari viongozi wa Yanga wanasuka
mipango ya kuvamia Ethiopia kuangalia nani anaweza kufiti kuingia kwenye kikosi
chao, lakini pamoja na hivyo wanakwenda na jina la mshambuliaji wa Stand
United, Elias Maguli kwa lengo la kuangalia kama ataendelea kuwa katika kiwango
chake ili wamalizane naye.
Maguli ambaye jana alidhihirisha kwamba yuko vizuri kwa kupachika mabao mawili kati ya manne yaliyoiwezesha
timu ya Taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars kuibuka na ushindi mnono wa
mabao 4-0 dhidi ya Somalia.
Maguli ameanza kuwindwa na klabu mbalimbali baada ya kuonyesha uwezo wa
hali ya juu kwenye michuano ya Ligi Kuu na mechi mbili za kuwania kufuzu
fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018, alipoifunga bao Taifa Stars dhidi ya
Algeria wakati walipotoka sare ya mabao 2-2 katika mchezo wa kwanza uliochezwa
Novemba 14 mwaka huu, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Alifunga bao ugenini na kukataliwa na mwamuzi katika mchezo wa pili
uliochezwa Algeria na wenyeji hao kuibuka na ushindi wa mabao 7-0.
Kutokana na kiwango kilichoonyeshwa na mshambuliaji huyo ambaye kwa sasa
anaongoza kwa ufungaji katika Ligi Kuu Bara baada ya kufunga mabao tisa,
imeelezwa Yanga wamemfungia safari hadi Ethiopia.
BINGWA limeelezwa kwamba baadhi ya vigogo wanataria kusafiri ndani ya
wiki hii, ambapo pamoja na Maguli pia watakuwa na kazi maalumu ya kuangalia wachezaji
wengine muhimu kwa mujibu wa mahitaji ya kocha.
“Ni kweli kuna watu watasafiri kwenda Ethiopia na huko watakuwa na kazi
maalumu ya kuangalia wachezaji, si lazima wale ambao tutawasajili hivi sasa
lakini pia kuweza tu kutambua nani anaweza kutufaa hata kwa baadaye,” alisema
mtoa habari wetu.
Pamoja na Maguli kuhusishwa na Yanga kwenye usajili huo, klabu nyingine
inayotajwa kuwania saini yake ni TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
(DRC).
Habari zilizolifikia gazeti la BINGWA zinaeleza kwamba, wajumbe kutoka
DRC wametua nchini kwa lengo la kumalizana na Maguli baada ya kuridhika na
kiwango alichokionyesha kwenye timu ya Taifa Stars na klabu yake.
Akizungumza na BINGWA kutoka Ethiopia, Maguli alisema anatarajia kuweka
wazi mpango baada ya kukamilika kwa usajili wake katika klabu inayomhitaji.
Maguli alisema kwa sasa suala zima litabaki kama lilivyo, lakini ataweka
kila kitu wazi baada ya kukamilika kwa dili lake.
“Kila mtu anasema lake mara naenda huku mara kule, lakini ukweli naujua
mimi mwenyewe, kwa sasa ni mchezaji wa Stand kama kutakuwa na timu naenda
kuitumikia nje ya hiyo nitaweka wazi mpango mzima hadharani,” alisema Maguli.
Maguli akiri kuhitajika na klabu mbalimbali lakini alisema ni mapema kuzitaja
kutokana na kwamba wanaendelea na mazungumzo na klabu hizo.- Chanzo kwa hisani ya Bingwa.
Maoni
Chapisha Maoni