Maguli, Bocco waiua Somalia
WASHAMBULIAJI wa timu ya taifa ya Tanzania Bara,
‘Kilimanjaro Stars’, John Bocco na Elias Maguli, wameiua Somalia baada ya
kufunga mabao mawili kila mmoja katika ushindi wa mabao 4-0 walioupata katika
mchezo wa Kundi A, wa Kombe la Chalenji uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Taifa wa Addis Ababa, Ethiopia.
Ushindi huo umewafanya Kilimanjaro Stars kuongoza
kutokana na idadi ya mabao ya kufunga baada ya Rwanda kuibuka na ushindi wa bao
1-0 dhidi ya wenyeji Ethiopia.
Katika mchezo wa jana, Bocco aliandika bao la
kuongoza katika dakika ya 12 kwa penalti baada ya beki wa kulia, Shomary
Kapombe kuangushwa eneo la hatari.
Kilimanjaro Stars waliandika bao la pili kupitia kwa
Maguli dakika ya 17 kabla ya Bocco kuongeza la tatu dakika ya 54.
Hata hivyo, Maguli alifunga hesabu baada ya kufunga
bao la nne na kukamilisha ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya wapinzani wao hao.
Kilimanjaro Stars iliundwa na Aishi Manula, Shomary
Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Kevin Yondan, Salum Mbonde, Himid Mao,
Simon Msuva/Malimi Busungu (dk71), Said Ndemla,
Bocco, Maguli na Deus Kaseke.
Timu hiyo inatarajia kucheza na Rwanda katika
mwendelezo wa michuano hiyo kesho Jumanne.
Katika mchezo mwingine, Kenya iliibuka na ushindi wa
mabao 2-0 dhidi ya Uganda uliochezwa kwenye uwanja huo.
Maoni
Chapisha Maoni