Read, Rotary wazipiga jeki shule ya msingi Msasani A&B
SHIRIKA lisilo la
kiserikali la Read International kwa kushirikiana na Chama cha Wafanyabiashara
wanaojitolea katika kusaidia jamii (Rotary), wamekabidhi maktaba kwenye shule
mbili za Msasani A na B jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuinua kiwango cha
elimu shuleni hapo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa maktaba hizo shuleni hapo, Mkurugenzi wa Read International, Montse Pejuan, alisema lengo la maktaba hizo ni kutaka kusaidiana na Serikali ili kuinua kiwango cha elimu nchini kwani Serikali peke yake haiwezi kufanya kila kitu.
“Kwa sasa kuna
sera ya Matokeo Makubwa Sasa (BRN) hivyo bila kushirikiana pamoja na Serikali
kamwe hatuwezi kufikia malengo ya sera hiyo ndio maana tumekuwa tukijaribu
kusaidia pale tunapoweza kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo,
lengo likiwa ni katika kuhakikisha kuwa shule zote zinakuwa na maktaba nchini,”
alisema Pejuan.
Naye Rais wa
Rotary Club of Dar Osterbay, Mohamed Versi, alisema hutoa misaada mbalimbali
kwa jamii hivyo walijitolea kwa moyo mmoja kuhakikisha wanashirikiana na Read
ili kuwezesha shule hizo kupata maktaba kwani pia ziko kwenye mazingira
yanayowazunguka.
“Sisi kama Rotary
huu ni mpango wetu wa kwanza kati ya tisa tuliyojiwekea katika kuhakikisha kuwa
tunasaidia jamii ya Watanzania kwenye nyanja mbalimbali za elimu, afya na maji,
hivyo chochote tunachokipata tumekuwa tukikifikisha kwa walengwa moja kwa moja
kupitia mahitaji mbalimbali,” alisema Versi.
Kwa upande wake,
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Msasani B, Egidious Mjunangoma, alisema msaada
huo wa maktaba utakuwa chachu ya kusaidia kuinua kiwango cha elimu na maendeleo
ya kitaaluma kwa wanafunzi wa shule hizo.
Naye Jennifer
Ruben wa Shule ya Msasani A, alisema awali walikuwa na vitabu kwenye stoo
lakini hawakuwa na maktaba hivyo uwepo wa maktaba hiyo utasaidia wanafunzi
kupata mwanya wa kuongeza maarifa zaidi.
Maktaba hizo
pamoja na vitabu vimegharimu zaidi ya Sh milioni 16 za Tanzania.
Maoni
Chapisha Maoni