Lowassa: Nimechoka kuitwa fisadi
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa jana aliwataka
wanaomhusisha na ufisadi kuacha mara moja kwa sababu hakuna hata chembe
ya ukweli katika tuhuma hizo.
Lowasa akizungukwa na waandishi dodoma |
Mbunge huyo wa Monduli alikuwa mmoja kati ya
makada tisa waliorudisha fomu jana, ikiwa ni siku moja kabla ya kuisha
kwa muda uliowekwa na chama hicho. Wengine waliorejesha fomu jana ni
Elidephonce Bilohe, Mwigulu Nchemba, Luhaga Mpina, Dk Hamisi
Kigwangalla, Hassy Kitine, Mariki Marupu, Dk Asha Rose Migiro na Lazaro
Nyalandu.
Nyalandu.
Hadi sasa, tayari wanachama 32 kati ya 42 wa CCM
walioomba kuteuliwa na chama hicho kugombea urais wamerudisha fomu na
kazi hiyo itahitimishwa leo.
Hakuna mtu ambaye amejitokeza hadharani kumtuhumu
Lowassa kwa ufisadi, lakini tuhuma hizo zimekuwa zikisambaa kwenye
mitandao ya kijamii, hasa kutokana na mbunge huyo wa Monduli kujiuzulu
nafasi ya Waziri Mkuu mwaka 2008 baada ya kuibuka sakata la mkataba wa
ufuaji umeme wa dharura baina ya Serikali na Kampuni ya Richmond RDC ya
Marekani ambayo ilionekana haina uwezo.
Wakati huo, Lowassa alisema kwenye hotuba yake ya
kujiuzulu kuwa amefanya uamuzi huo “ili kuonyesha dhana ya uwajibikaji,
lakini kutokubaliana na utaratibu uliotumika wa kusema uongo ndani ya
Bunge kwa kumsingizia mtu.”
Akizungumza jana kwenye ofisi za makao makuu ya
CCM, Lowassa alirudia wito wake wa kutaka wenye ushahidi wa tuhuma hizo
wajitokeze hadharani.
“Nataka nitumie fursa hii kuwataka wale wote ambao
wamekuwa wakinituhumu kwa miaka kadhaa sasa na kunihusisha na suala
zima la rushwa, nawaambia waache mara moja, kwani hakuna chembe hata ya
ukweli wa maneno hayo,” alisema.
“Natoa changamoto kwa yeyote mwenye ushahidi wa
tuhuma hizo za kipuuzi, autoe na aeleze kwa ushahidi rushwa yoyote
inayonihusu, aseme nimechukua lini, kwa nani, kwa lipi na kiasi gani?”
Alisema yeye ni mwadilifu na anaposema atasimamia
vita dhidi ya rushwa atafanya hivyo kwa vitendo bila kumuonea mtu na
bila kumuonea haya yeyote.
“Ndugu wanachama wenzangu na wananchi kwa jumla,
ni lazima sasa tufike mahali tuseme imetosha. Majungu yametosha,
upotoshwaji umetosha, rushwa imetosha na kwa pamoja tunaweza kukomesha
haya. Tutayakomesha kwa kusimamia ukweli, uadilifu, uaminifu na kutenda
kwa haki,” alisema.
Ukumbi wa Whitehouse, jana ulijaa wana-CCM ambao
walifika kushuhudia Lowassa akirudisha fomu tofauti na idadi iliyowahi
kutokea kwa wagombea wengine kadhaa waliomtangulia. Hali hiyo
ilisababisha foleni kwenye Barabara ya Mtaa wa Kuu unaopita mbele ya
ofisi za CCM, na kusababisha usumbufu kwa wapita njia.
Mwananchi
Mwananchi
Maoni
Chapisha Maoni