Yanga yawapeleka Simba Msuva, Niyonzima
KLABU ya Yanga imesema kuwa
haiumizwi kichwa na tetesi za watani wao wa jadi Simba kuwamendea wachezaji wao,
Haruna Niyonzima na Simon Msuva kwani wana uwezo wa kuziba mapengo yao.
Mikataba ya Niyonzima na Msuva
inatarajiwa kufikia tamati mwishoni mwa msimu huu na wamekuwa wakihusishwa na
mpango wa kutua Simba.
Tayari Mwenyekiti wa Kamati ya
Usajili Simba, Zacharua Hanspoppe, ameweka wazi kuwa lazima wamsajili Msuva
kwani nyota huyo ana kila alichoita ‘damu ya Msimbazi’, yaani ni mpenzi wa
klabu yao yenye maskani yake Mtaa wa Msimbazi.
Akizungumza Dar es
Salaam , Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro,
alisema Yanga ni klabu kubwa ambayo inafanya mambo yake kisasa ndiyo maana
hawababaiki na uvumi huo, akiweka wazi kuwa wachezaji hao wana haki ya
kuzungumza na timu yoyote.
“Yanga tunaendesha mambo yetu
kitaalamu zaidi wala hatukurupuki kama wengine, lakini pia kwa habari ya
kuzungumza na mchezaji, hata mimi naweza kufanya hivyo kwa yeyote, hivyo Simba
kuzungumza na Msuva na Niyonzima wala halina presha kwetu.
“Kwa kipindi hiki akili yetu ipo
kwenye kuutangaza ubingwa mapema na pia namna ya kuwakabili Etoile du Sahel,
hivyo tunawaambia mashabiki wetu waelekeze akili zao huko, haya mengine wala
yasiwatie wasiwasi,” alisema.
Juu ya suala zima la usajili, alisema
hawawezi kukurupuka na badala yake wanasubiri mapendekezo ya kocha wao Van der Pluijm
kujua nani anamtaka na nani hamuhitaji.
“Hatuwezi kufanya jambo ambalo
hatujaambiwa na benchi letu la ufundi chini ya kocha wetu Hans kwani kufanya
hivyo ni sawa na kumuingilia majukumu yake,” alisema.
Msuva ametokea kuwa mchezaji muhimu
katika kikosi cha Yanga, akiwa anaongoza orodha ya wafungaji ambao katika mechi
za Ligi Kuu Bara baada ya kufunga mabao 14.
Maoni
Chapisha Maoni