Twite nje ‘First 11’ Yanga SC
MBUYU Twite ameanza kuona chungu ya kugombana na
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Hans van der Pluijm baada ya jana kutupwa nje ya
kikosi cha kwanza cha timu hiyo inayojiandaa kucheza na Ruvu Shooting leo
katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mchezo huo utakuwa ni muhimu mno kwa Yanga kwani
iwapo itashinda, itakuwa imejisogeza karibu zaidi na ubingwa wa ligi hiyo na
itafikisha pointi 52, ikibakiza pointi tatu kutangaza ubingwa.
Azam ndiyo wanaoshika nafasi ya pili katika ligi
hiyo wakiwa na pointi 42, wakiwa wamebakiza mechi nne na iwapo watashinda zote,
watafikisha pointi 54.
Na kuelekea mchezo wa leo wa Yanga, kikosi hicho
jana asubuhi kilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, ambapo
Twite hakuwapo katika kikosi cha kwanza.
Kikosi hicho cha kwanza cha leo kiliundwa na kipa
Ally Mustapha ‘Barthez’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Rajab Zahir, Kelvin Yondani,
Said Juma, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe, Kpah Sherman na Mrisho
Ngassa.
Katika mazoezi hayo, Twite alikuwa upande wa
wachezaji wa akiba sambamba na wachezaji wengine nyota kama Andrey Coutinho,
Hussein Javu, Jerry Tegete na Salum Telela pamoja na Nadir Haroub ‘Cannavaro’
ambao ni majeruhi.
Zahir inaonekana leo ataanza katika beki ya kati
pamoja
na Yondani baada ya Cannavaro kuumia katika mchezo wao Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Etoile du Sahel wiki iliyopita.
na Yondani baada ya Cannavaro kuumia katika mchezo wao Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Etoile du Sahel wiki iliyopita.
Japo Pluijm hakuwa tayari kumzungumzia Twite, habari
za ndani zinasema kuwa mchezaji huyo amemkera mno kocha huyo kutokana na
kujibizana naye Jumanne ya wiki hii baada ya mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi
ya Stand United kwenye Uwanja wa Taifa.
Pluijm baada ya mchezo huo alimfokea Twite kwa
kuboronga na kuwawezesha wapinzani wao hao kupata mabao mawili, japo
Wanajangwani hao walishinda 3-2.
Baada ya mchezo, Twite alikaririwa akielezea jinsi
alivyokerwa na kocha huyo, akidai yupo tayari kuondoka Yanga iwapo klabu hiyo
itaendelea kumlea kocha huyo.
Ni wazi kuwa kauli hiyo ya Twite itakuwa imezidi
kuuchochea moto Jangwani juu ya majaliwa yake ndani ya kikosi hicho,
ikizingatiwa Pluijm ametokea kuwa kipenzi cha watu wa Yanga.
Maoni
Chapisha Maoni