Safari yamkuta Twite Yanga
BEKI wa Yanga mwenye uwezo wa kucheza nafasi nyingi,
Mbuyu Twite amejikuta njiapanda ndani ya kikosi cha timu hiyo baada ya kutoa
kauli iliyowakera viongozio wake.
Juzi Twite alitofautiana na Kocha Mkuu wa Yanga, Hans
van der Pluijm baada ya Mholanzi huyo kumkoromea mchezaji wake kwa madai ya
kuboronga katika mchezo wa siku hiyo dhidi ya Stand United kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Yanga walishinda mabao 3-2 na kuzidi kujichimbia
kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania, lakini waliocheza chini ya
kiwango, ikiwa ni pamoja na safu ya ulinzi iliyokuwa chini ya Twite kupoteana.
Hali hiyo, hasa kuruhusu kufungwa mabao mawili
ilimkera mno Pluijm ambaye anaheshimika kwa soka la kushambulia, lakini pia
akiwa na safu imara ya ulinzi.
Baada ya mchezo huo, Pluijm alimwita Twite na
kumfokea hadharani akifanya hivyo pia kwa kipa Deogratius Munishi ‘Dida’.
Kitendo hicho
kilionekana kumuumiza Twite na kutishia kuondoka ndani ya kikosi cha timu hiyo
kilichopo kambini kwenye Hoteli ya Tansoma, jijini.
Lakini Twite alifika mbali kwa kusema kuwa Yanga
wanatakiwa kuchagua mawili, aidha kumtema Pluijm ili yeye aendelee kubaki, au
aondoke yeye kocha huyo aendelee kupeta Jangwani.
“Kwanini anifokee hadharani mbele za watu wakati si
mimi niliyefanya makosa? Siwezi kukubali, ni heri niondoke Yanga kocha abaki au
aondoke yeye mimi nibaki,” alisema.
BINGWA lilimtafuta Mkuu wa Idara ya Habari na
Mawasiliano ya Yanga, Jerry Muro kuzungumzia suala hilo ambapo alikana kuwapo
kwa mgongano kati ya kocha wao na wachezaji hao.
“Hakuna walichokuwa wanagombana isipokuwa kocha
alikuwa anamtania na kumuuliza maana juzi (Jumatatu) walinunuliwa vifaa vipya
na kila mmoja alitakiwa kuwa navyo, lakini yeye (Twite) hakuja navyo ndiyo
akamuuliza kwa utani kuwa aliviacha wapi,” alisema Muro.
Pamoja na utetezi huo wa Muro, BINGWA linatambua
kuwa Twite atakuwa amelikoroga Yanga kutokana na kauli yake ‘ni heri niondoke
Yanga kocha abaki au aondoke yeye mimi nibaki’, kutokana na ukweli kuwa Pluijm
amekuwa kipenzi cha Wanayanga zaidi ya hata ilivyo kwa mchezaji yeyote yule wa
timu hiyo.
Ni wazi ni suala la kusubiri na kuona kama si
kusikia nini kitafuata baada ya kauli na msimamo huo wa Twite.
Lakini kwa hali ilivyo, iwapo Twite atazidi kuwa
ngangari juu ya msimamo wake huo, huenda siku zake ndani ya Yanga zikafikia
kikomo kwani ni wazi hakuna mtu yeyote ndani ya klabu hiyo atakayekuwa tayari kumuona
Pluijm akiondoka Jangwani kwa sababu ya mchezaji kama Twite.
Maoni
Chapisha Maoni