Okwi: Nina machungu na Azam
Mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi (jezi nyekundu) akiwapiga chenga wachezaji wa Mgambo Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu Vodacom Tanzania Bara.Picha na Michael Matemanga |
MSHAMBULIAJI
wa kimataifa wa Simba, Mganda, Emmanuel Okwi anaisubiri kwa hamu Azam FC baada
ya juzi kufunga hat-trick dhidi ya JKT Mgambo katika mchezo wa marudiano wa
Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika
mchezo huo ulichezwa kwenye uwanjani hapo, Simba walishinda mabao 4-0 na
kufikisha pointi 38 wakiwa nyuma ya Yanga wenye pointi 49 na Azam FC (42).
Akizungumza
na juzi, Okwi alisema ushindi huo ni salamu tosha kwa timu wanazotarajia
kucheza nazo ikiwemo ya Azam ambao wanawania nao nafasi mbili za juu ili waweze
kushiriki michuano ya kimataifa.
Okwi
alisema kwa sasa akili yake ipo katika kuiwezesha timu yake kuvuna pointi tatu
kwenye mechi zao zote tatu zilizobaki.
“Nafikiria
kushinda michezo yote iliyobaki na baada ya hapo tutajua tutakuwa kwenye nafasi
gani, kama ni ya pili au la,” alisema Okwi.
Pamoja na
kutokwenda kiundani zaidi, Okwi anaonekana kuwa na hasira zaidi na Azam ambao
katika mchezo wa mzunguko wa kwanza baina ya timu hizo, Mganda huyo alijikuta akiwa
katika wakati mgumu baada ya kuchezewa rafu mbaya.
Beki wa
kati wa Azam, Agrey Morris, ndiye aliyemchezea rafu hiyo kwa kumpiga kiwiko
hali iliyomfanya mchezaji huyo kupoteza fahamu.
Kwa
inavyoonekana, kitendo hicho kilimuuma mno Okwi hivyo kuona njia pekee ya
kulipiza kisasi ni kuipiga mabao Azam watakapokutana nayo kama alivyowafanyia
Mgambo JKT juzi kwa kuwafunga matatu peke yake katika ushindi wa 4-0.
Wakati
Okwi akisema hayo, Kocha Mkuu wake, Goran Kopunovic alisema kihesabu Simba
wanaweza kushika nafasi ya pili itakayofanya washiriki michuano ya Kombe la Shirikisho
barani Afrika mwakani.
Kopunovic
alisema lengo lake ni kutaka kuendelea kuifundisha timu hiyo, iwe kwenye
kiwango cha juu na washinde michezo iliyosalia ingawa katika soka lolote
linaweza kutokea.
Alisema wanajipanga katika
kuhakikisha wanashinda mchezo unaofuata dhidi ya Ndanda
FC utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa
kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Ndanda FC walipoteza kwa Simba baada ya
kufungwa mabao 2-0.
Maoni
Chapisha Maoni