Mcameroon wa Yanga ni habari nyingine
YOUSSOUF Sabo aliyetua
Yanga ambaye ni mdogo wake kiungo hatari wa Etoile du Sahel ya Tunisia, Franck Kom,
ameanza mazoezi na kuonyesha vitu adimu kiasi cha kumtoa udenda beki kisiki wa
timu hiyo, Oscar Joshua.
Katika mazoezi hayo
yaliyofanyika Uwanja wa Karume, Dar es Salaam jana asubuhi, Sabo alionyesha
kuwa na nguvu mno akiwa si mwoga wa kupambana kiasi cha kumtoa jasho Joshua
anayesifika kwa soka la ubabe.
Mbali ya sifa hiyo
ambayo ndiyo iliyowatesa washambuliaji wa Yanga walipovaana na Etoile mwishoni
mwa wiki iliyopita na kuambulia sare ya bao 1-1, Sabo ameonyesha kuwa na uwezo
mkubwa wa kumiliki mpira kuanzia upokeaji wake wa pasi, jinsi anavyoficha mpira
na hata kutoa pasi.
Kwa jinsi anavyoonekana,
iwapo atazoeana na wenzake ikiwa ni pamoja na kujiona kama sehemu ya timu ya
Yanga, anaweza kuwa moto wa kuotea mbali kutokana na kuwa na sifa zote
anazostahili kuwa nazo mchezaji mpambanaji.
Juu ya vita yake na
Joshua jana, mara ya kwanza Sabo alimchukulia beki huyo ‘kishkaji’, lakini
wakati akiuwahi mpira mwenzake huyo alimvaa na kumtoa kwenye njia na kuuchukua
mpira.
Kuona hivyo, Mcameroon
huyo alijibu mapigo ambapo baada ya kupata mpira, aliumiliki na Joshua
alipofika ‘alimpa upaja’ na beki huyo wa kushoto kupepesuka, hali iliyowakosha
mashabiki waliokuwapo wakishuhudia mazoezi hayo.
Mchezaji huyo alimtoa
jasho Joshua zaidi ya mara tatu, jambo ambalo huwa ni nadra kufanywa na
mchezaji yeyote ndani ya kikosi cha Yanga dhidi ya beki huyo mwenye mwili
uliojengeka vilivyo.
Baada ya mazoezi hayo,
Sabo alipongezwa na nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, lakini pia
Kocha Mkuu wa timu hiyo Mholanzi, Hans van der Pluijm.
Pluijm alionekana
akiteta na mchezaji huyo huku akimshika kichwa katika hali ya kuonyesha
kumkubali.
BINGWA lililokuwa
likimfuatilia kwa makini mchezaji huyo tangu mwanzo wa mazoezi hayo,
lilizungumza na kocha huyo kutaka kujua kama ameguswa na Sabo, ambapo alisema:
“Ni mchezaji mzuri, lakini nahitaji muda wa wiki tatu kumfahamu vizuri.”
Pluijm alisema kuwa
baada ya muda huo, atajua kama Sabo atafaa kuwapo katika kikosi chake cha msimu
ujao au la.
Jumamosi kwenye Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam baada ya mchezo kati ya Yanga na Etoile, Sabo alionekana
kiwa na Kom ambapo waliteta kwa takribani dakika tano kisha kila mmoja
‘kuchukua hamsini zake’.
Akizungumza na BINGWA
uwanjani hapo siku hiyo, Sabo alisema kaka yake huyo alimsisitizia kutofanya
makosa iwapo atapata nafasi ya kuichezea Yanga.
Kabla ya kukutana na
Kom, waandishi wa habari wa Tunisia na baadhi ya wachezaji wa Etoile,
walionekana kumshangaa Sabo kuwapo uwanjani pale ambapo walimfuata na kumsalimu
na kupiga naye picha.
Sabo amemaliza mkataba
wake na klabu ya Cotton Sports ya Cameroon, akiwa ni nahodha wa timu ya Taifa
ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (U-20) wa nchi hiyo.
Juu ya jinsi alivyokiona
kikosi cha Yanga siku ile, alisema: “Nimewaona wachezaji wa Yanga wanavyocheza,
wapo wenye uwezo lakini wengine hakuna kitu, mfano uliona ati mchezaji
unawekewa mkono unaanguka kirahisi na kuuachia mpira! Katika soka hakuna kitu
kama hicho, unatakiwa kupambana kwa akili na nguvu zako zote si kujilegeza,”
alisema Sabo.
Katika mazoezi ya jana,
Pluijm aliweka mkazo zaidi katika suala zima la umakini kwa wachezaji wake, kutoa
pasi zinazofika kwa walengwa kwa wakati na nafasi sahihi, lakini pia kutokabia
kwa macho.
Yanga wanajiandaa na
mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting utakaopigwa Uwanja
wa Taifa leo, lakini pia ule wa marudiano dhidi ya Etoile wa Kombe la
Shirikisho Afrika Mei Mosi, mwaka huu nchini Tunisia.-bingwa
Maoni
Chapisha Maoni