JK kuzindua kitabu cha muungano
RAIS Jakaya Kikwete, kesho ijumaa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kitabu kinachoelezea
historia ya miaka 50 ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar.
RAIS Jakaya Kikwete |
Akizungumza Dar es Salaam
jana, mwandishi wa kitabu hicho kilichopewa jina la ‘Photographic
Journey’, Javed Jafferji amesema lengo la kuaandaa kitabu hicho ni kuonesha
matukio muhimu ambayo Tanzania imepitia tangu nchi hizo zilipoungana mwaka
1964.
“Tumepitia mambo mengi, bado tumeendelea kudumisha
ushirikiano wetu, tukaona ipo haja ya kuyaweka kwa pamoja ndani ya kitabu ili
kuwasaidia wale ambao hawajui waweze kuyajua,” alisema.
Amesema kitabu hicho ambacho kina kurasa 444, kinaelezea
historia ya viongozi mbalimbali waliopita, Azimio la Arusha, ujenzi wa reli ya
TAZARA na vita ya Kagera.
“Kitabu hiki ni cha kwanza na kina baraka zote za marais wetu wa pande zote
mbili, kitasaidia watu kufahamu historia mbalimbali ndani ya Tanzania pia
kitaweza kutumika mashuleni pamoja na kuutangaza utalii wa ndani,”amesema
Jafferji.
Kwa upande wake, mwandishi na mhariri wa kitabu hicho,
Simai Said amesema upo umuhimu wa kuweka kumbukumbu vizuri kwa ajili ya manufaa
ya kizazi kijacho.
“Katika uandaaji wa kitabu hiki tumetumia picha mbalimbali
ambazo zinaelezea matukio tofauti tofauti yaliyotokea ndani ya kipindi cha kati
ya mwaka 1964 hadi 2014 lakini tulitumia muda wa zaidi ya miezi 17
kuzipata,”amesema Javed.
Amesema uzinduzi huo utahudhuriwa na watu mbalimbali ambao
wameandikwa ndani ya kitabu hicho ikiwa ni sehemu ya kuutambua mchango wao
walioutoa kwa Taifa, akiwamo Mtanzania wa kwanza na mwafrika wa pili kupanda
mlima Evarest ambao ni mrefu kuliko yote
duniani.
Maoni
Chapisha Maoni