IPTL kujenga zahanati Kawe
KAMPUNI ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL),
ambayo ni kampuni tanzu ya Pan Africa Power Solutions (T) Limited (PAP),
inatarajia kujenga zahanati katika Kata ya Kawe, ili kupunguza tatizo la
upatikanaji wa huduma za afya kwa wakazi wanaozunguka kampuni hiyo.
Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu
na Mshauri Mkuu wa Sheria wa kampuni hiyo, Joseph Makandege, wakati
akikabidhi msaada wa vyandarua 700 vyenye thamani ya Sh milioni 10 katika
Zahanati ya Wazo na zahanati nyingine zilizopo katika kata za Kunduchi na Kawe.
Amesema msaada huo ambao unalenga kuunga mkono maadhimisho ya Siku
ya Malaria duniani, umetolewa sasa ili kusaidiana na jamii katika jitihada za
kupambana na ugonjwa huo.
“Tumeanza kuchangia katika vita dhidi ya malaria na baada ya hapa
tunatarajia kuwa na mradi mkubwa wa afya katika Kata ya Kawe, tumeanza
mazungumzo na viongozi wa Kata ya Kawe ili kuona uwezekano wa kujenga zahanati.
“Hii ni moja kati ya maeneo ambayo Mwenyekiti Mtendaji
wetu, Harbinder Singh Sethi na bodi kwa pamoja wameuelekeza uongozi wa IPTL/PAP
kujikita zaidi katika awamu hii ya kwanza ya utekelezaji wa mpango mkakati wetu
wa uchangiaji katika shughuli za kijamii,” alisema.
Aidha, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya
Kinondoni, Paul Makonda, Diwani wa Kata ya Wazo, John Moro (CCM), aliipongeza
kampuni hiyo kwa kuwajali wananchi katika vita dhidi ya ugonjwa huo.
“Msaada wenu kwa wananchi wa Kinondoni ni kielelezo cha
ukaribu wenu kwa jamii ya Watanzania katika kusaidia na kukuza maendeleo nchini.
Katika miaka kadhaa sasa malaria imeendelea kuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo
ya Taifa kutokana na kusababisha vifo vya nguvu kazi ya Taifa na watoto
wachanga ambao kimsingi ndio Taifa la kesho.
Aidha, mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Ruth Mahmood,
pamoja na kuishukuru kampuni hiyo kuwapatia msaada huo, pia aliiomba serikali
iandae makakati wa ujenzi wa jengo la wazazi ambalo litakuwa likitoa huduma
zote ili kupunguza adha kwa akina mama wajawazito pindi wanapotaka kujifungua.
Maoni
Chapisha Maoni