yanga yaitunishia TP Mazembe kwa Ngassa
UONGOZI wa Yanga umeikata maini TP Mazembe ya
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) iliyoonyesha nia ya kumtwaa mshambuliaji
wao hatari, Mrisho Ngassa, ikisema kamwe haiwezi kumwachia kirahisi nyota wao
huyo.
Ngassa ni miongoni mwa wachezaji wa Yanga ambao
mikataba yao inamalizika mwishoni mwa msimu huu na tayari mkali huyo alielezea
azma yake ya kuondoka Jangwani baada ya kumalizika kwa mkataba wake.
Wakati wapenzi wa Yanga wakiwa njiapanda juu ya
majaliwa ya nyota wao huyo iwapo ataendelea kuwa nao au la, uongozi wa wakongwe
hao wa soka nchini umevunja ukimya kwa kuweka wazi kuwa wapo tayari kutoa kiasi
chochote cha fedha kumbakisha mchezaji mwenye mchango mkubwa na timu yao wa
kiwango cha Ngassa.
Kauli hiyo ilitolewa wiki iliyopita na Katibu Mkuu
wa Yanga, Jonas Tiboroha, alipokuwa akizungumza na BINGWA juu ya majaliwa ya
wachezaji wao wanaoelekea kumaliza mikataba yao akiwamo Ngassa.
Alisema wamejipanga kuhakikisha wanawabakiza
wachezaji wao nyota, ikiwa ni pamoja na kuboresha baadhi ya vipengele kwenye
mikataba yao kutokana na kutambua michango yao ndani ya timu.
Aliongeza wachezaji wote ambao wana msaada ndani ya
Yanga, kamwe hawatapewa nafasi ya kuondoka kirahisi, hasa katika kipindi hiki
ambacho mikakati yao ni kuzidi kutamba katika anga la kimataifa na michuano ya ndani
pia.
“Hakuna mchezaji ambaye ana msaada kwa timu yetu
tutamruhusu kuondoka hapa, wale wanaomaliza mikataba na ambao hawajamaliza hatuwezi
kuwaruhusu wakaondoka kirahisi,” alisisitiza Tiboroha.
Alisema kwa sasa wanaangalia jinsi ya kuboresha
mazingira ya wachezaji wao katika kila idara ili kuwawezesha kujituma zaidi na
kuitumikia timu hiyo kwa uwezo na nguvu zao zote.
Alisisitiza wana mipango endelevu lukuki, zaidi
ikiwa ni kutamba kimataifa, hivyo ili kuitimiza wanahitaji kuwa na kikosi
kilichokaa pamoja kwa muda mrefu.
“Hakuna sababu ya wale wanaomaliza mikataba yao au
waliobakiza muda mfupi kuanza kuzungumza kwenye vyombo vya habari, watulie
mambo mazuri yanakuja, tumejipanga kuhakikisha wanafurahia maisha ndani ya
Yanga,” aliongeza.
Baadhi ya wachezaji wa Yanga ambao mikataba yao
imebakisha muda mfupi kumalizika ni Mbuyu Twite, Haruna Niyonzima, Deogratius
Munishi ‘Dida’, Ngassa na Amissi Tambwe.
Hivi karibuni, Ngassa alisema anataka kuondoka Yanga
kwani anahisi kutothaminiwa, japo baadaye aliibuka na kutaka dau la Sh milioni
100 ili aweze kubaki Jangwani.
Yanga kwa sasa ipo katika nafasi nzuri ya kutwaa
ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kwani hadi sasa inaongoza ligi hiyo ikiwa na
pointi 37 baada ya kucheza mechi 18, huku ikiwa imejiwekea mazingira mazuri ya
kutinga raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuichapa FC
Platinum ya Zimbabwe mabao 5-1 katika mchezo wa kwanza.
Timu hizo zitarudiana Aprili 3, mwaka huu nchini
Zimbabwe ambapo Yanga watatakiwa kushinda au kupata sare yoyote waweze kusonga
mbele.
Wakati huo huo, mshambuliaji wa Yanga, Amissi
Tambwe, ataukosa mchezo wa kesho dhidi ya JKT Ruvu kutokana na kutumikia adhabu
ya kadi tatu za njano alizoonyeshwa kwenye michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Yanga itashuka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kesho
kuwavaa JKT Ruvu, huku ikimkosa mfungaji wao huyo ambaye mwishoni mwa wiki
iliyopita alifunga bao katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mgambo JKT kwenye
Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.-Bingwa
Maoni
Chapisha Maoni