Yanga: majeshi yote Ligi Kuu

YANGA SC imeweka kando kwa muda fikra za michuano ya kimataifa na sasa silaha zake za maangamizi inazielekeza kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo leo imeapa kuifanyia kitu mbaya Kagera Sugar.
Mabingwa hao mara 24 wa Ligi Kuu wanaingia katika mchezo huo wakiwa na ari ya ushindi wa mabao 5-1 walioupata mwishoni mwa wiki dhidi ya FC Platinum Stars ya Zimbabwe, katika michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

 
Yanga watakuwa wenyeji wa Kagera Sugar katika mchezo unaotarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, huku timu hiyo ikipania kuwashushia kipigo cha mbwa mwizi wakata miwa hao, ikiwa ni kutaka kulipiza kisasi cha kufungwa katika mechi ya mzunguko wa kwanza.
Timu hizi zilipokutana mzunguko wa kwanza, Kagera Sugar waliibuka na ushindi wa bao 1-0, lililowekwa kimiani na straika Paul Ngwai, ambapo Yanga chini ya Kocha Hans Pluijm, imeapa kulipiza kisasi ili kupata pointi tatu muhimu kwa ajili ya kujiweka sawa katika mbio za ubingwa.
Kwa sasa safu ya ushambuliaji ya Yanga ni moto wa kuotea mbali, kutokana na kutumia vema nafasi wanazozipata tofauti na awali ambapo Pluijm ameweka wazi kuwa anafurahishwa na jinsi vijana wake wanavyofuata maelekezo.
Kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Mrisho Ngassa, ambaye msimu uliopita alikuwa mmoja wa wachezaji walioibuka vinara kwenye michuano ya Klabu Bingwa Barani Afrika, amekwishakwamisha mabao sita na kurejea kwenye moto wake, akishirikiana na Simon Msuva pamoja na Amis Tambwe.
Hata safu ya ulinzi nayo chini ya Nadir Haroub ‘Cannavaro’, pamoja na Kelvin Yondani inaonekana kuwa imara, kwani ndiyo pekee iliyoruhusu mabao tisa ambayo ni machache tofauti na timu nyingine.
Yanga baada ya kufungwa na Simba bao 1-0, wameonekana kuwa na hasira za kushinda idadi kubwa ya mabao kwa kila timu inayojipendekeza mbele yao.
Dhamira ya Yanga msimu huu ni kurejesha ubingwa ambao unashikiliwa na Azam FC, ambao waliwapoka msimu uliopita ambapo kocha Pluijm amewahimiza wachezaji wake kukaza buti.
Yanga wanaingia katika mchezo wa leo wakiwa nafasi ya pili na pointi zao 31 walizozipata baada ya kushuka uwanjani mara 16, huku wapinzani wao wa jadi, Simba wakiwa nafasi ya tatu na pointi 29.

Kwa upande wao Kagera Sugar, chini ya kocha wao Mkuu Mganda, Jackson Mayanja, wametamba kwamba Yanga wasitarajie mteremko, kwani hata wao wanahitaji pointi tatu ili kumaliza Ligi wakiwa moja ya nafasi za juu.
Wakatamiwa hao wako nafasi ya nne nyuma ya Simba, wakiwa na pointi 25 baada ya kushuka dimbani mara 18, ambapo kama watafanikiwa kuibuka na ushindi leo, watazidi kujitengenezea mazingira mazuri ya kuwakaribia walioko juu yao.
Katika mchezo wa leo, Yanga itawakosa nyota wake sita kutokana na sababu mbalimbali.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro, ambaye alizungumza kwa niaba ya kocha Pluijm, wachezaji wanne kati yao watakosekana kutokana na kutumikia adhabu ya kadi za njano na wawili ni majeruhi.
Jerry aliwataja wachezaji hao kuwa ni Kelvin Yondani, Haruna Niyonzima, Danny Mrwanda na Said Juma, ambao wanatumikia adhabu ya kadi tatu za njano, huku nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub 'Cannavaro' na Andrey Coutinho wakiwa bado ni majeruhi.
Alisema, baada ya mechi hiyo kikosi cha Yanga kinatarajiwa kwenda Tanga Alhamisi kwa ajili ya mchezo wao dhidi ya Mgambo Shooting, utakaochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkwakwani.-Dimba

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HADITHI:MWALIMU MAGDALENA sehemu ya 1

Hadithi: Mwalimu Magdalena sehemu ya 5

Hadithi: Mwalimu Magdalena sehemu ya 4