Sserunkuma avunja mkataba

HABARI mpya ndani ya Simba ni kwamba straika wao raia wa Uganda, Dan Sserunkuma, ameomba kuvunja mkataba mwishoni mwa msimu kwa kile kilichoelezwa kuchoka kukaa benchi na kuhatarisha kiwango chake.
Mbali na hilo, pia uongozi wa Simba unaendelea kufanya mabadiliko katika nafasi mbalimbali za viongozi na juzi Jumanne ulitangaza kumtoa Humphrey Nyasio katika nafasi ya Ofisa Habari na badala yake amechukuliwa na Haji Manara, huku ikielezwa kuwa wapo mbioni kumbadili Katibu Mkuu wake, Stephen Ally dhidi ya Hamis Kisiwa.
Habari kutoka ndani ya Simba, zinasema kuwa Dan ambaye bado yupo kwao Uganda kwa matatizo ya kifamilia, aliwatumia ujumbe viongozi wake kuwaomba kuvunja mkataba wake ligi itakapomalizika kwani utakuwa umebakiza mwaka mmoja na nusu.
Simba ilimsajili Dan akitokea Gor Mahia ya Kenya akiwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Kenya msimu uliopita akifunga mabao 16.
Klabu hiyo ilimpa mkataba wa miaka miwili, hivyo mpaka ligi itakapomalizika atakuwa ametumikia miezi sita tu.
“Dan bado hajarudi kutoka kwao, aliomba ruhusa kuwa ana matatizo ya kifamilia, alitakiwa awe amerudi toka wiki iliyopita lakini ametuma taarifa ya kutaka kuvunja mkataba wake ambayo bado haijajadiliwa, sidhani kama kutakuwa na pingamizi kwani hajaonyesha kiwango tulichotarajia,” kilisema chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Simba.
“Mikataba ya wachezaji wa kigeni ipo wazi baada ya kufanyiwa marekebisho kwamba mchezaji akishindwa kufikisha malengo ya kuisaidia timu basi mkataba wake unaweza kuvunjwa.”
Kocha wa Simba, Goran Kopunovik amekuwa akimwanzisha benchi straika huyo aliyeifungia timu hiyo mabao matatu, kwa kile kilichodaiwa kuwa bado hajaridhishwa na kiwango chake.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe alisema: “Sina taarifa hizo, ninachofahamu ni kwamba alipewa ruhusa ya kwenda kutatua matatizo ya kifamilia ingawa alitakiwa awe amerudi toka Jumamosi iliyopita ila mpaka sasa hajarudi.”
Wakala wa mchezaji huyo, Ken Joseph alisema kuwa ni kweli Dan hajarudi Simba licha ya ruksa aliyopewa na uongozi kumalizika, lakini suala lake limeshamalizwa baina ya pande hizo.
Katika hatua nyingine,beki wa kigeni wa Simba, Joseph Owino amesema bado hajaamua hatma yake ndani ya klabu hiyo mpaka hapo Ligi Kuu Bara msimu huu itakapomalizika.
Owino ni mmoja wa nyota wa Simba wanaomaliza mikataba yao mwishoni mwa msimu ambapo ameliambia Mwanaspoti kuwa itategemea kama abaki Simba au arejee kwao Uganda.
“Itategemea hapo baadaye, ila ikitokea klabu ikanipa ofa nzuri nitabaki Bongo,” alisema beki huyo aliyewahi kuichezea Azam miaka ya nyuma. Kwa muda mrefu sasa, Owino amekuwa hapati nafasi kikosi cha kwanza. -mwanasport

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HADITHI:MWALIMU MAGDALENA sehemu ya 1

Hadithi: Mwalimu Magdalena sehemu ya 5

Hadithi: Mwalimu Magdalena sehemu ya 4