Simba stamina asilimia 100%

Kocha wa Simba Goran Kopunovic
SIMBA imepata kiburi baada ya timu hiyo kuonyesha matumaini makubwa kufuatia stamina ya hali ya juu pamoja na soka safi iliyoanza kuonekana tangu ujio wa kocha Goran Kopunovic na kuifanya ionekane kuwa ni moto wa kuotea mbali.
Awali timu hiyo ilikuwa ikionekana dhaifu na kupata matokeo mabovu kutokana na kukosa stamina na pumzi ya kutosha, lakini sasa imekamilisha vitu hivyo kwa asilimia 100.

Simba ilikuwa ikicheza vizuri dakika 45 tu za kipindi cha kwanza, huku kipindi cha pili ikionekana kukosa stamina na pumzi, lakini sasa tatizo hilo linaonekana kumalizika ambapo kocha wake, Kopunovic atakuwa akitaka kuonyesha kuwa kikosi chake kimeiva kwenye mchezo wa leo dhidi Maafande wa Mgambo JKT, jijini Tanga.
Katika michezo yao ya hivi karibuni, Wekundu hao wa Msimbazi wameonekana kuhimili dakika zote 90 na kufanikiwa kuibuka na ushindi kiasi cha kujitengenezea mazingira mazuri ya kuaminika kwa mashabiki wake ambao awali walikuwa na wasiwasi inapofikia kipindi cha pili.
Wekundu hao wameonyesha kuiva tangu mchezo dhidi ya watani zao wa jadi, Yanga, uliomalizika kwa ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Emmanuel Okwi, ambapo walihimili dakika zote 90 kabla ya kufanya yao mwishoni mwa wiki iliyopita dhidi ya Mtibwa kwa kuichapa bao 1-0.
Tatizo la kukosa stamina na pumzi kwa wachezaji wa Simba limekuwa la muda mrefu, lakini sasa Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Goran Kopunovic, amelifanyia kazi na kama wataendelea hivyo wanaweza wakaibuka na ushindi mwingine leo dhidi ya Mgambo JKT, katika Uwanja wa Mkwakwani.http://shaffihdauda.co.tz/wp-content/uploads/2015/02/IMG_0522.jpg
Simba wanataka kuendeleza wimbi la ushindi leo dhidi ya wenyeji wao, Mgambo JKT na kuwadhihirishia mashabiki wake kuwa hawakuwafunga Yanga na Mtibwa Sugar kwa bahati mbaya.
Katika mchezo wa leo, Simba watamtegemea zaidi mshambuliaji wao hatari, Mganda Emmanuel Okwi, ambaye amekuwa gumzo kubwa kutokana na aina ya mabao anayoyafunga, likiwamo alilofunga dhidi ya Yanga na lile dhidi ya Mtibwa Sugar.
Matokeo mazuri waliyoyapata katika michezo yao hiyo ya hivi karibuni yameweza kuwafanya wasimame kwenye nafasi ya tatu wakiwa na pointi 29 nyuma ya Azam na watani zao wa jadi, Yanga-dimba

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HADITHI:MWALIMU MAGDALENA sehemu ya 1

Hadithi: Mwalimu Magdalena sehemu ya 5

Hadithi: Mwalimu Magdalena sehemu ya 4