Mwanafunzi asimulia alivyoruka ghorofani
MWANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Cecilia Mosha
(26) aliyejirusha kutoka ghorofa ya tatu hadi chini kutokana na hofu ya moto uliotokea
katika Hosteli ya Mabibo, amevunjika mfupa wa bega.
Mwanafunzi huyo alijirusha kupitia dirishani juzi katika
harakati za kujiokoa na moto baada ya jengo la wasichana, Block A kushika
moto huku wanafunzi wakiwa vyumbani wakiendelea na shughuli zao.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Cecilia ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Shahada ya
Uhandisi wa Uchimbaji Madini, alisema alisikia kelele akiwa chumbani na alipotoka
nje akakuta moshi umetanda kila kona.
“Baada ya kuona hivyo niliona ni vema nijiokoe kwa
kujirusha kutoka ghorofa ya tatu ya bweni hilo hadi chini kupitia
dirishani,”alisema Mosha.
Alisema baada ya kuruka hadi chini alikimbizwa katika kituo
kidogo cha afya karibu na hosteli hiyo
ambako alipoteza fahamu na kushtukia yupo katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa
ya Fahamu Muhimbili (MOI).
Naye Meneja Ustawi na Uhusiano wa Taasisi ya MOI, Almasi Jumaa
alisema hali ya Cecilia si mbaya na anaendelea na matibabu.
“Tumempokea huyo mgonjwa jana na baada ya timu ya madaktari
kumfanyia vipimo vya kutosha wamebaini amevunjika mfupa wa bega la kulia na kupata
mshtuko wa mwili … alipata maumivu ya kiuno na mwili kwa ujumla,” alisema
Jumaa.
Ajali hiyo ya moto ilitokea juzi katika Hosteli ya Mabibo
iliyopo Mtaa wa Ubungo Kibangu, Dar es
Salaam.
Kwa mujibu wa Makamu
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala moto
huo uliteketeza ghorofa ya tatu ya jengo A linalotumiwa na wanafunzi wa kike.
Alisema moto huo haukuwa na madhara kwa binadamu ingawa
uliteketeza mali za wanafunzi.
Profesa Mukandali aliahidi uongozi wa chuo utahakikisha
wanafunzi hao wanapata msaada wa hali na mali.-mtanzania
Maoni
Chapisha Maoni