Msuva atimukia Simba
WINGA wa Yanga, Simon Msuva, amesema kuwa baada ya
kumalizika kwa mkataba wake, atafungasha virago vyake Jangwani na kutua Mtaa wa
Msimbazi yalipo maskani ya Simba ili kujiepusha na lawama dhidi yake.
Mkataba wa mchezaji huyo Yanga umeelezwa kutarajiwa
kumalizika mwishoni mwa msimu huu.
Akizungumza na BINGWA hivi karibuni, Msuva alisema pamoja
na kuipenda Yanga, amejikuta katika wakati mgumu kutokana na shutuma dhidi
yake, hasa pale anapocheza chini ya kiwango.
Alisema kuwa tangu alipotua Jangwani, amekuwa
akicheza kwa uwezo wake wote ili kuisaidia timu yake, lakini anapokosea hata
kwa bahati mbaya mashabiki wa timu hiyo humtukana bila sababu za msingi wakidai
eti ana mapenzi na Simba.
“Siku zote nimekuwa nikijituma kadiri ya uwezo wangu
kuisaidia timu yangu ya Yanga, lakini nikikosea hata kwa bahati mbaya huwa ni
shida, sasa ni kheri niende kutafuta maisha kwingineko, iwe ni Simba au hata
Azam kwani ninachoangalia ni masilahi,” alisema.
Msuva alisema japo katika familia yao wengi ni
wapenzi wa Simba, kwa upande wake amekuwa akiitumikia Yanga kwa mapenzi yake
yote kwani ndiyo klabu iliyolikuza jina lake, akitamani kupata mafanikio
makubwa akiwa na klabu hiyo.
Winga huyo mwenye mbio, alijikuta akiwa katika
wakati mgumu Yanga ilipocheza na Simba pale mashabiki wao walipodai kuwa
alikuwa akicheza chini ya kiwango kutokana na mapenzi yake kwa Wekundu wa
Msimbazi hao.
Kati ya vitu vilivyomponza mchezaji huyo, ni kitendo
chake cha kukosa mabao mawili akiwa katika nafasi nzuri, ikiwamo pasi fyongo
aliyotoa akiwa ndani ya sita na mpira kuokolewa na mabeki wa Simba.
Hata katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika
dhidi ya Platinum ya Zimbabwe Jumapili iliyopita, Msuva alijikuta matatani
akidaiwa kucheza chini ya kiwango kama ilivyokuwa Jumatano ya wiki hii
walipoivaa Kagera Sugar kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Juu ya tishio hilo la Msuva kuondoka Jangwani, Mkuu
wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Yanga, Jerry Muro, alisema kuwa kimsingi
klabu yao imekuwa ikiwathamini mno wachezaji wake, lakini kwa yeyote anayetaka
kuondoka hawatamzuia iwapo atakuwa amefuata taratibu.
“Hatuwezi kumzuia mchezaji yeyote atakayetaka
kuondoka katika timu hii, Yanga imekuwapo muda mrefu na kuna wachezaji wengi
wamepitia hapa na kuiacha kama ilivyokuwa,” alisema Muro, mmoja wa wasemaji
matata na wenye mbwembwe nyingi wa klabu za soka hapa nchini.
Msuva ndiye mchezaji wa Yanga mwenye mabao mengi
zaidi katika orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu Bara, akiwa amecheka na nyavu mara
nane, akizidiwa mabao mawili na kinara, Didier Kavumbagu.-Bingwa
Maoni
Chapisha Maoni