Mserbia Simba nianga nyingine
KOCHA Mkuu wa Simba, Goran Kopunovic, ameelezea
kufarijika kwake kwa kufanikiwa kwa kiasi kikubwa katika mafundisho yake ya
kufunga mabao ya ‘move’, hivyo kuamua kugeukia kuyafanyia kazi mabao ya adhabu.
Miongoni mwa mabao hayo ya adhabu, ataweka mkazo
zaidi katika kufundisha jinsi ya kufunga kwa vichwa mipira ya kona, krosi na
adhabu kutoka pembeni mwa uwanja, mtindo uliompa umaarufu gwiji wa Uholanzi,
Patrick Kluivert, wakati akizitumikia timu mbalimbali, ikiwamo kikosi chao cha
Taifa.
Enzi zake, Kluivert alikuwa ni mahiri wa kufunga
mabao ya vichwa kutokana na mipira ya kona, krosi na adhabu kutoka pembeni mwa
uwanja.
Akizungumza na BINGWA jana, Goran alisema amebaini
kuwa mabao mengi ambayo timu yake imefunga, yamekuwa yakitokana na ‘move’
zilizoanzia iwe katikati ya uwanja au pembeni.
“Ukiangalia mabao mengi ambayo tumekuwa tukifunga,
yametokana na move, hivyo nimeona nigeukie kufanyia kazi mipira ya adhabu
pamoja na kona ili wachezaji wangu wafunge bao,” alisema.
Goran alisema kulingana na mipira ya adhabu na kona
imekuwa tatizo na kusababisha kutopata ushindi, sasa anawatengeneza wachezaji
wake katika kufunga katika mipira ya kona na adhabu.
“Kikosi changu kimeonyesha kiwango kizuri sana,
nimeridhishwa na jinsi walivyocheza, lakini bado kuna kazi naifanyia hasa
kuhakikisha mipira ya adhabu na kona inazaa matunda,” alisema kocha huyo.
Alisema atakapofanikiwa kufanya vyema katika mipira
hiyo ya adhabu na kona ana imani hatapata tabu katika viwanja vibaya kama kile
cha Mkwakwani walipopoteza pointi muhimu dhidi ya Mgambo JKT.
“Ukiangalia Uwanja wa Mkwakwani sio mzuri, hivyo
uwanja kama ule unatakiwa kufunga kwa njia ya kona au mipira ya adhabu, hilo
ndilo lilitukwamisha kwani ukiangalia zaidi wachezaji wangu wanafunga mabao kwa
move,” alisema kocha huyo.
Simba inatarajia kucheza na Ndanda FC ya Mtwara,
Jumamosi ya wiki ijayo kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.-Bingwa
Maoni
Chapisha Maoni