Bao 5 za Yanga zazidi kuitesa FC Platinum
YANGA imeonekana kuitia mkosi FC Platinum ya
Zimbabwe, baada ya timu hiyo kutoka sare ya mabao 2-2 na Dongo Sawmills katika
mchezo wa Ligi Kuu ya nchi hiyo uliochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita nchini
humo.
Katika michezo mitano FC Platinum walikuwa
hawajapoteza kabla ya kufungwa na Yanga mabao 5-1 katika mchezo wa kwanza wa
raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho barani Afrika hivi karibuni kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wapinzani hao wa Yanga walikuwa na mwenendo mzuri
katika ligi ya kwao, ikiwa iliichapa Chicken Inn mabao 2-0 Novemba 3, mwaka
jana, kabla ya kuipiga bao 1-0 Hwange
Novemba 9, mwaka jana na baadaye kuendelea kutoa
vipigo kwa kuifunga Chiredzi mabao 3-0 Novemba 23 mwaka jana.
Wazimbabwe hao waliwagekia Sofapaka ya Kenya na kuwafunga
mabao 2-1 katika mchezo wa awali wa Kombe la Shirikisho Februari 15, mwaka huu,
nchini Kenya.
FC Platinum walipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Sofapaka
katika mchezo wa marudiano uliochezwa Machi mosi mwaka huu na kufanikiwa kuvuka
hatua
iliyofuata ya michuano hiyo.
Hata hivyo, FC Platinum walipata kibano baada ya
kufungwa na
Yanga mabao 5-1 katika mchezo uliochezwa Machi 15
mwaka
huu, kwenye Uwanja wa Taifa.
Timu hiyo kabla ya kurudiana na Yanga Aprili 3,
mwaka huu wanatarajia kucheza na Caps United Jumamosi.
Kwa matokeo hayo, FC Platinum wanashika nafasi ya
sita katika msimamo wa ligi hiyo, huku Dynamos wakiwa kileleni wakifuatiwa na
ZPC Kariba.-Bingwa
Maoni
Chapisha Maoni