Yanga yatua Mbeya kibabe
BAADA ya Yanga kuifunga BDF XI ya Botswana mabao 2-0
katika mchezo wa kwanza wa raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika Jumamosi
ya wiki iliyopita, timu hiyo inaondoka Dar es Salaam kwenda Mbeya tayari kwa mechi
zao dhidi ya Prisons na Mbeya City, huku wakiwa na matumaini makubwa ya
kushinda.
Katika mchezo wao dhidi ya BDF XI uliopigwa kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga ilicheza vizuri mno na iwapo
washambuliaji wake wangekuwa makini, wangevuna zaidi ya idadi hiyo ya mabao.
Ushindi wa Jumamosi unaonekana kuzidi kuwapandisha
mzuka Yanga ambapo wameapa kuvamia Jiji la Mbeya kwenda kuendeleza furaha yao
katika mechi mbili za Ligi Kuu Tanzania Bara zitakazopigwa Uwanja wa Sokoine Alhamisi
na Jumapili.
Katika mchezo wao wa kwanza jijini humo, watamenyana
na Prisons Alhamisi, kabla ya kushuka dimbani tena Jumapili kukipiga na Mbeya
City.
Mechi hizo zote ni ngumu ambapo iwapo watashinda,
watakuwa wamejiweka katika mazingira mazuri kwenye msimamo wa ligi hiyo, kwa
sasa wakiwa wanashika nafasi ya pili nyuma ya Azam, japo timu zote hizo kila
moja ina pointi 25 na mechi 13, lakini zikizidiana kwa wastani wa mabao ya
kufunga na kufungwa.
Wakati huo huo, kikosi cha Yanga kinatarajia
kuondoka nchini Februari 25, mwaka huu kuekelea Botswana tayari kwa mchezo wa
marudiano dhidi ya BDF XI utakaopigwa kati ya Februari 27 na Machi mosi, mwaka
huu.
“Mara baada ya kumaliza michezo yetu miwili ya ligi jijini
Mbeya, tunatarajia kurejea Dar es Salaam Jumatatu kujiandaa na safari ya
Botswana siku inayofuata,” alisema Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh.-bingwa
Maoni
Chapisha Maoni