Wenye ulemavu watoa masharti Uchaguzi Mkuu
CHAMA cha Walemavu Tanzania (Chawata), kimewataka wanasiasa
kuandaa wakalimani katika mikutano yao ya kampeni katika Uchaguzi Mkuu
unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu ili waweze kushiriki vyema na kufanya
uamuzi wa kuchagua viongozi sahihi kwa maendeleo ya taifa.
Mwenyekiti wa walemavu Amoni Mpanju |
Mbali na hilo, pia wamewataka wanasiasa kutumia maandishi
ya nukta nundu pamoja na yaliyokuzwa maalumu kwa watu wenye ulemavu wa ngozi
(albino) na wale wasioona vizuri katika vitabu vya ilani zao za uchaguzi.
Hayo yalisemwa kwenye mkutano wa watu wenye ulemavu jijini
Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa chama hicho, Amon Mpanju, wakati wa uwasilishaji wa waraka kwa wadau wa
demokrasia nchini.
Mpanju alisema lengo ni kuwa na ushiriki mpana na wenye
tija kwa watu wenye ulemavu katika michakato yote ya demokrasia nchini.
Alisema wamefikia uamuzi huo baada ya kuwapo kwa ushiriki
mdogo wa walemavu katika michakato ya kidemokrasia na utawala wa nchi kama raia
wengine.
“Sisi raia wa nchi
hii wenye ulemavu tunataka tuhakikishiwe
kupata haki sawa katika kuchagua au kuchaguliwa kwenye ngazi zote za uchaguzi
hapa nchini,” alisema Mpanju.
Maoni
Chapisha Maoni