Wanafunzi kinondoni kupata vyeti vya kuzaliwa mashuleni

Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) unategemea kuanza rasmi mkakati wa kuwasajili na kuwapa vyeti vya kuzaliwa wanafunzi wa shule za Msingi za Manispaa ya kinondoni Ijumaa wiki ijayo tarehe 27 Februari 2015 ambapo mpango huu utatekelezwa katika shule 140 zenye wanafunzi wapatao 155,944. Lengo ni kusajili wanafunzi 20,000.
Kuzinduliwa kwa mkakati huu katika Manispaa ya Kinondoni ni muendelezo wa mkakati mkuu uliozinduliwa Mwezi Aprili 2014 unao wawezesha wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari kusajiliwa na kupata vyeti vya Kuzaliwa katika shule wanazosoma.

Katika mkakati huu kila shule huteua mwalimu mmoja atakayeratibu zoezi baada ya kupewa mafunzo ya kina kuhusu Usajili wa Vizazi na kupewa vitendea kazi kwa ajili ya kufanya usajili wa awali katika shule zao. Baada ya Mwalimu kuwatangazia wanafunzi na wazazi kuhusu huduma hiyo kupatikana shuleni atagawa fomu za maombi kwa wanaohitaji na atahakiki fomu zilizojazwa na atazikusanya na kuziwasilisha fomu RITA kwa ajili ya kuhakikiwa na kuandaliwa vyeti. Mara baada ya vyeti kukamilishwa hupelekwa kwa mwalimu ambaye atavigawa kwa wanafunzi husika.
Tayari mkakati huu umeshaanza kutekelezwa katika Manispaa ya Ilala jijini Dar es salaam umeshafanyika katika shule 105 za Msingi na 96 za Sekondari za Manispaa ya Ilala na kuonyesha mafanikio Makubwa na Zaidi ya wanafunzi 16,000 wa mesajiliwa nakupata Vyeti vya kuzaliwa. Kati ya hao 51.2% Ni wavulanana 48.8% ni wasichana. Usajili katika manispaa ya Ilala bado unaendelea.
Chimbuko la Mkakati huu ni uhitaji mkubwa wa Nyaraka hii Kutokana na mfumo wa Elimu kusisitiza Cheti cha kuzaliwa kuwa nyaraka inayothibitisha umri wa mwanafunzi mara anapotoka hatua moja ya elimu kwenda inayofuata.
Baada ya kukidhi vigezo mwanafunzi hupata cheti kwa kufuata mfumo wa kawaida wa uhakiki ili kuhakikisha ni wale wanaostahili tu ndio wanaopata vyeti vya kuzaliwa.Wanafunzi watakao sajiliwa ni wale waliozaliwa katika Mkoa wowote wa Tanzania Bara na watatakiwa kuwa na viambatanisho kama Tangazo la Kizazi, kadi ya Kliniki, Cheti cha Ubatizo, Cheti cha Falaki, Pasi ya kusafiria na watakaokosa vyote kati yavilivyotajwa kutakuwa na utaratibu maalumu utakaowekwa ili kuwawezesha nao kupatacheti cha kuzaliwa.
RITA ina amini wazazi wa wanafunzi wanaosoma katika shule za Msingi katika Manispaa ya Kinondoni watatumia fursa hii kuwasajili watoto ili wapate vyeti vya kuzaliwa. Cheti cha kuzaliwa ni nyaraka muhimu kwa kila mwananchi kwani humwezesha mwanafunzi kuweza kupata nafasi za masomo ya sekondari na baadae elimu ya juu, kupata mikopo ya elimu, kufungua akaunti ya Benki, kupata huduma za Afya kupitia mifuko ya jamii, kupata pasi ya kusafiria na matumizi mengineyo.

Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano (RITA)

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HADITHI:MWALIMU MAGDALENA sehemu ya 1

Hadithi: Mwalimu Magdalena sehemu ya 5

Hadithi: Mwalimu Magdalena sehemu ya 4