Wachezaji Yanga wajazwa manoti
UONGOZI wa Yanga umefikia uamuzi wa kuboresha
mishahara ya wachezaji wao, kutokana na kile kinachoonekana kufurahishwa na
mwenendo wa kikosi chao katika Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho
Afrika.
Yanga inashika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi
Kuu Bara, lakini ikiwa na pointi 25 na mechi 13 sawa na vinara Azam waliopo
kileleni kutokana na wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Katika michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho,
timu hiyo imeanza kwa mbwembwe kwa kuichapa BDF XI ya Botswana mabao 2-0 katika
mchezo wa kwanza wa raundi ya awali uliopigwa Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam.
Ukiachana na ushindi huo, moyo wa kupambana
unaoonyeshwa na wachezaji wa timu hiyo, ndio hasa unaoushawishi uongozi wa
Yanga kufikiria jinsi ya kuwafurahisha zaidi vijana wao waweze kufanya mambo
makubwa zaidi wakiamini hilo lipo ndani ya uwezo wao.
Juu ya mpango wao huo wa kuboresha mishahara ya
wachezaji, uongozi wa klabu hiyo umeona ni vema wakafanya hivyo pale
wanapokunwa na kandanda au ushindi wa timu yao badala ya kuwaahidi kuwapa fedha
kama ilivyokuwa awali.
Hayo yote yanaonekana kulenga katika kuwapandisha
mzuka wachezaji wao waweze kupambana kadiri ya uwezo wao, ili kuisambaratisha
BDF XI katika mchezo wa marudiano, lakini pia kuzipiku Azam na Simba kwenye
mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Akizungumza na BINGWA, Katibu Mkuu wa Yanga, Jonas
Tiboroha ambaye ni mtaalamu wa masuala ya ukocha na ufundi, alisema hawana sababu
ya kuwaahidi fedha wachezaji pindi wanapokuwa na mechi ngumu zaidi ya
kuwaboreshea posho na mishahara yao.
“Hatuna sababu ya kuwaahidi fedha kila wanapokuwa na
mechi ngumu, kushinda mchezo ni sehemu ya majukumu yao, hivyo ndiyo maana
utaona kuna baadhi ya vitu tumeviboresha,” alisema Tiboroha.
Alisema kila mchezaji anapaswa kuwajibika, kujituma
na kujitolea kwa ajili ya timu na masilahi yake binafsi iwe ni ndani ya Yanga
au kwingineko.
Hata hivyo, kiongozi huyo hakuwa tayari kuweka wazi
kwamba watawaongezea mishahara wachezaji wao kwa kiasi gani na ni vigezo gani
watakavyovitumia katika hilo.
Lakini BINGWA linatambua kuwa ongezeko la mishahara
kwa wachezaji, litategemea na mchango wa mchezaji husika, wale watakaokuwa wakijituma
na kuisaidia zaidi timu ndio watakaoneemeka zaidi.-bingwa
Maoni
Chapisha Maoni