Ubakaji wampeleka jela maisha
MKAZI wa Kata ya Igulubi wilayani Igunga mkoani
Tabora, Sudi Seif (47), amehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa
kosa la ubakaji.
Seif alihukumiwa jana na Mahakama ya Wilaya ya
Igunga.
Awali mwendesha mashitaka wa Serikali, Elimajid
Emmanuel, akimsomea mashtaka ya mtuhumiwa mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya
ya Igunga, Ajal Milanzi, alisema Aprili 16 hadi Juni 16 mwaka 2014, kwa nyakati
tofauti, Seif aliwabaka na kuwaingilia kinyume na maumbile watoto wawili, mmoja
mwenye umri wa miaka sita na mwingine tisa.
Alidai kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo na
kuwasababishia maumivu makali watoto hao, jambo ambalo ni kinyume na kifungu
cha 130, kifungu kidogo cha kwanza cha kanuni ya adhabu kilichofanyiwa
marekebisho mwaka 2002 kinachozuia kutenda makosa kama hayo.
Baada ya kusomewa mashtaka, Seif alikana
kutenda makosa hayo na ndipo upande wa
mashtaka ulipeleka mashahidi watano ambao walitoa ushahidi mahakamani.
Baada ya
kusikiliza ushahidi kutoka pande zote mbili, Hakimu Milanzi alisema pasipo
shaka mahakama imemwona mshtakiwa ana hatia, hivyo inamwadhibu kutumikia
kifungo cha maisha jela ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama
hiyo.
Maoni
Chapisha Maoni