Traore, Wanga mdomoni mwa Simba
SIMBA wamewateka washambuliaji hatari wa mabingwa wa
Sudan El-Merreikh, Mohamed Traore na Allan Wanga ambao juzi walikuwa mwiba mchungu
kwa mabeki wa Azam, wakati wa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa
Uwanja wa Azam Complex, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, Azam ilishinda mabao 2-0, lakini
mabeki wake, hasa Muivory Coast, Pascal Wawa, wakifanya kazi ya ziada
kumdhibiti Wanga aliyecheza dakika zote 90.
Baada ya mchezo huo, Makamu wa Rais wa Simba,
Geoffrey Nyange ‘Kaburu’, hakutaka kufanya kosa na kujitosa ‘mzima mzima’
kwenda kufanya mazungumzo na Wanga.
BINGWA lilimshuhudia Kaburu akizungumza na Traore na
baadaye Wanga, lakini ikiwa ni baada ya kiongozi huyo kuwapongeza wawili hao
kwa kazi waliyoifanya.
Simba ilishawahi kumtaja Traore kama mmoja wa
wachezaji waliokuwa katika mpango wao wa usajili wa dirisha dogo la Desemba
mwaka jana.
Baada ya kuzungumza na Kaburu, BINGWA lilimfuata
Wanga kutaka kujua alichokuwa akiteta na bosi huyo wa Simba, ambapo alisema: “Ninafahamiana
naye (Kaburu) kwani tulikutana Kenya pamoja na Zanzibar nilipokuwa na timu ya
AFC Leopards katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi mwaka jana.”
Alipoulizwa iwapo yupo tayari kutua Simba, alisema
kuwa hilo linawezekana kwani mchezaji yeyote huwa anaangalia masilahi, hivyo
kama Wekundu wa Msimbazi hao watakuwa tayari kumlipa kiasi anacholipwa El Merreikh,
hana shida.
Gazeti hili jana lilimtafuta Kaburu kujua alichoteta
na washambuliaji hao ambapo alisema: “Ni kweli nilizungumza na wachezaji wote
wawili, hii si mara ya kwanza kukutana nao, kimsingi tunawahitaji kwani ni wachezaji
wazuri.”
Aliongeza: “Nilisamehe kwenda Morogoro kuisapoti
timu yangu ya Simba ikicheza na Polisi Moro kwa ajili ya kukutana na Traore na
Wanga na kila kitu kimekwenda kama tulivyotaka.”
Alisema atakutana na wenzake akiwamo Mwenyekiti wa
Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspoppe, kuanza mchakato wa kuwasajili
wachezaji hao mwishoni mwa msimu wakiamini hakuna linaloshindikana, hasa baada
ya kufahamu mustakabali wao ndani ya El Merreikh.
“Lengo letu ni kuifanya Simba kuwa tishio, hivyo
tutaiimarisha zaidi safu ya ushambuliaji kwani matarajio yetu ni kushiriki
michuano ya kimataifa mwakani kwani uwezo huo tunao baada ya kupanda hadi
nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Bara,” alisema Kaburu.
Simba iliyoanza Ligi Kuu Bara kwa kusuasua, imeanza
kucharuka na kuchupa kutoka nafasi ya tisa hadi ya nne, ikiwa na pointi 20, nyuma
ya vinara Azam na Yanga.-bingwa
Maoni
Chapisha Maoni