Precision kuuza ndege zake
SHIRIKA la Ndege la Precision linatarajia kuuza baadhi ya ndege zake na
kubakiza ndege sita kupunguza mzigo wa
madeni yanayoikabili Kampuni hiyo kwa sasa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa shirika
hilo, Michael Shirima alisema Dar es Salaam jana kuwa hatua hiyo imefikiwa kutokana na uchakavu wa
ndege hizo na hali ya uchumi wa kampuni.
“Kampuni iko katika mazungumzo na mwekezaji ili kukamilisha
makubaliano ya kununua ndege zenye madeni na kisha kuzikodisha kwa kampuni
nyingine… makubaliano haya yanatarajiwa kufikiwa mwishoni mwa robo ya kwanza ya
mwaka huu,” alisema Shirima.
Alisema pamoja na kufikia hatua hiyo kampuni haijakata
tamaa kwa kuweka jitihada ya kutafuta
mtaji mkubwa kupitia kwa wanahisa wa sasa au wawekezaji wasio wanahisa.
Awali akiitoa taarifa katika mkutano mkuu wa mwaka wa Tatu wa wanahisa,
Shirima alisema mazingira ya biashara yalikuwa na ushindani huku kukiwa na hofu
juu ya usalama duniani kote.
Pia alisema thamani ya fedha za kigeni hususan Dola ya
Marekani imeendelea kukua ikilinganisha na shilingi ya Tanzania hivyo
kusababisha akiba hafifu ya fedha za kigeni na hasara kwa biashara ambazo
matumizi yake mengi yanategemea fedha hizo.
Maoni
Chapisha Maoni