Nabii atabiri machafuko nchini
Nicolaus Suguye |
NABII Nicolaus Suguye wa Kanisa la The Word of
Reconciliation Ministries (WRM) iliyopo Matembele ya Pili jijini Dar es Salaam,
ametabiri nchi kuingia kwenye machafuko kutokana na uvamizi wa maadui kutoka
nje ya nchi ambao watasababisha baadhi ya Watanzania kupoteza maisha kutokana
na mapigano yatakayozuka.
Kauli hiyo aliitoa mwishoni mwa wiki iliyopita
wakati wa ibada kanisani hapo na kuwataka waumini wote kuingia kwenye maombi ya
kufunga na kuomba ili kunusuru hali hiyo isijitokeze na kusababisha Watanzania
kuishi maisha ya wasiwasi, ambayo hawajayazoea tangu nchi hii ipate uhuru wake mwaka
1961.
“Nimeona maputo baharini yanatoka pande nne za dunia
kuja nchi kavu na yalikuwa yanamwaga sumu kali na kila aliyekuwa anagusa alikufa
na wengine walikatika viungo vyao na wengine walikimbia ovyo kwa lengo la
kutaka kuokoa maisha yao.
“Hii ina maana kuna hali ya machafuko ambayo
yataipata nchi hii, hivyo tunatakiwa kusimama kwenye maombi kwa ajili ya
kubatilisha hali hiyo,” alisema Nabii huyo.
Katika maombi ya siku saba, Nabii Suguye aliwataka
waumini hao kuyaombea majeshi yote ya Tanzania pamoja na viongozi wake, ili
Mungu awape macho ya kuona hali ya hatari iliyo mbele yao na kuwapa maarifa ya
kubaini wapi maadui walipojificha kwenye mipaka ya nchi.
Mtumishi huyo wa Mungu aliwataka Watanzania wote
bila kujali itikadi za siasa, kuendelea kuombea hali hiyo isijitokeze na siku
zote maombi huombwa wakati wa amani badala ya kusubiri machafuko yajitokeze
ndipo watu waanze kufanya hivyo na watakuwa wamechelewa.-MTANZANIA
Maoni
Chapisha Maoni