Mmoja afariki dunia baharini, wawili wanusurika Zanzibar
KIJANA mmoja amefariki
dunia na wengine wawili wamenusurika baada ya ajali ya kuzama kwa dau baharini
walilokuwa wakilitumia kuvulia samaki katika Kijiji cha Uzini, Shehia ya
Ng’ambwa, Wilaya ya Kati Unguja.
Akithibitisha tukio hilo,
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusin Unguja, Juma Saadi Khamis, alisema tukio hilo
lilitokea Februari 17, mwaka huu katika Kijiji cha Ng’ambwa ambapo vijana
watatu; Suleiman Asaa Suleiman (16), Alnoor Mohamed Issa (18) na Kassim
Masoud (14) walikuwa wakitumia chombo cha uvuvi aina ya dau katika bahari ya
kati, lakini ghafla hali ya hewa ilibadilika na chombo chao kikapinduka na
kuzama.
Dhoruba hiyo
ilisababisha kijana mmoja kati ya hao aliyetambuliwa kwa jina la Suleiman kupotea
ambapo wenzake walinusurika baada ya kushika sehemu za bembeni za dau hilo
lililokuwa limebinuka hadi walipopita wavuvi na kuwasaidia kuwarudisha kijijini
kwao.
Kamanda huyo ambaye ni
Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi Zanzibar, alieleza kuwa baada ya
wanakijiji kupata taarifa za kupotea kwa kijana huyo, walichukua juhudi za
kumtafuta katika eneo la bahari ambapo Februari 18 saa 10:00 jioni kijana huyo
aliokotwa akiwa amefariki dunia na mwili kukabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili
ya taratibu za mazishi.
Maoni
Chapisha Maoni