Kigogo CCM afia mkutanoni
MWAKILISHI wa Magomeni
visiwani Zanzibar, Salmin Awadhi Salmin (CCM), amefariki dunia ghafla baada ya
kuanguka katika kikao cha Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilichokuwa kinafanyika
katika ofisi kuu ya chama hicho, Kisiwandui mjini Unguja.
Mwili
wa Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni Salmin Awadh ukitolewa katika hospitali ya
Mnazimmoja Unguja kupelekwa nyumbani Mpendae baada ya mwakilishi huyo kufariki
ghafla akiwa kwenye kikao cha CCM Zanzibar jana. Salmin pia ni Mnadhimu Mkuu wa
Baraza la Mapinduzi na mjumbe wa kamati kuu wa chama cha mapinduzi |
Taarifa hiyo ilianza
kuenea mjini Unguja jana saa 6 mchana, na hata kuzua maswali kutoka kwa
wananchi kuhusu utata wa kifo chake.
Salmin (57) ambaye pia
alikuwa ni mnadhimu wa wawakilishi wa CCM na mjumbe wa Kamati Kuu ya chama
hicho (CC), alikuwa mmoja wa wawakilishi wanaopinga mfumo wa Serikali ya Umoja
wa Kitaifa (SUK) kwa kutaka wananchi waulizwe kama bado wanahitaji muundo huo
wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Akizungumza
na MTANZANIA kuhusu kifo cha mwakilishi huyo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar,
Vua Ali Vuai, alisema kabla ya kufikwa na mauti, alianguka ghafla wakati
akitoka katika kikao hicho cha kawaida.
Alisema
baada ya kuanguka viongozi na wanachama walimnyanyua na kumkimbiza Hospitali ya
Mnazi Mmoja kwa ajili ya matibabu.
“Baada
ya Salmin kuanguka, baadhi ya viongozi na wafanyakazi kwa haraka walimbeba na
kumpeleka katika Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa ajili ya matibabu na baada ya kufikishwa alipelekwa katika chumba cha
wagonjwa mahututi (ICU), ambako baada ya muda mfupi madaktari walithibitisha
kuwa amefariki dunia kwa maradhi ya shinikizo la damu.
“CCM
imepokea kwa mshtuko mkubwa kifo cha kiongozi wetu ambaye alikuwa ni kiongozi
na mtendaji wa kuigwa ndani na nje ya chama chetu, ila kazi ya Mungu haina
makosa, jambo la kusikitisha amefariki akiwa katika utendaji wa kazi za chama
hapa ofisi kuu Kisiwandui,” alisema Vuai.
Naibu
Katibu Mkuu huyo wa CCM alisema kwa sasa taratibu za mazishi zinaandaliwa na Serikali
kwa kushirikiana na chama nyumbani kwake Mpendae na anatarajiwa kuzikwa leo kijijini kwao Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja saa 7
mchana.
Kwa
upande wake, Katibu wa Baraza la Wawakilishi (BLW), Yahya Khamis Hamad, alisema
baraza hilo limeondokewa na kiongozi mahiri ambaye muda wote alikuwa na kazi ya
kuimarisha umoja kwa Wazanzibari.
Salmin
Awadh Salmin alizaliwa mwaka 1958 kisiwani Unguja na kusoma Shule ya Msingi
Makunduchi kabla ya kuwa kiongoni Wilaya ya Kusini Unguja.
Pia
amewahi kushika wadhifa mbalimbali ndani ya CCM ikiwamo ujumbe wa NEC, Kamati
Kuu na Mnadhimu wa Wawakilishi wa Kambi ya CCM ndani ya Baraza la Wawakilishi.
Machi
2, mwaka jana wakati wa mkutano wa Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma, Salmin
aliwaongoza wawakilishi wa CCM kupinga hatua ya Spika wa Baraza la Wawakilishi,
Pandu Ameir Kificho, kuwasilisha maoni kwa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba ya kutaka Serikali tatu na kuyaita ni maoni ya baraza hilo.
Katika
mkutano huo, Salmin alisema mapendekezo hayo ni kinyume na msimamo wa CCM na
wao hawako tayari kuliona hilo huku akiahidi suala hilo kufikishwa katika vikao
vya ngazi za juu.
Salmin
alisema Spika Kificho hakuwashirikisha wenzake katika mapendekezo ya Serikali
tatu aliyoyawasilisha kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, wakisema Baraza la
Wawakilishi, kama taasisi, halikutoa msimamo wa pamoja.
Mei 4, mwaka jana, Salmin
alisema wawakilishi wa CCM wanajiandaa kuwasilisha hoja binafsi kwenye Baraza la
Wawakilishi ili kuwapa nafasi wananchi waulizwe iwapo wanataka kuendelea na
Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), au la.
Kauli hiyo aliitoa
wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa chama hicho ulioongozwa na Katibu Mkuu
wake, Abdulrahman Kinana kwenye viwanja vya Kibandamaiti, Unguja.
Salmin alisema wajumbe
hao wamefikia hatua hiyo kwa kuwa wanaona kwamba lengo na matumaini ya kuundwa SUK
yamefutika na hayana dalili njema katika siku za usoni.
Alisema
ni vyema wananchi wakaulizwa kama bado wana hamu na mfumo huo au ule wa zamani
urejeshwe.
Katika
mkutano huo, alimwomba Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, kuunga mkono
hoja hiyo itakapowasilishwa ili kutoa nafasi mpya ya kidemokrasia kwa wananchi
wake kujua kama wanataka mfumo wa sasa au wa zamani.-MTANZANIA
Maoni
Chapisha Maoni