Albino aliyeporwa kwa mama yake auawa
MWILI wa mtoto albino, Yohana Bahati (mwaka mmoja) aliyeporwa kutoka
mikononi mwa mama yake katika Kijiji cha Lumasa, Wilaya ya Geita, Mkoa wa
Geita, umepatikana.
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Geita, Joseph Konyo, aliliambia MTANZANIA jana
kuwa mwili huo ulipatikana jana katika Pori la Hifadhi ya Biharamulo lililoko
Wilaya ya Biharamulo, Mkoa wa Kagera, ukiwa umenyofolewa mikono na miguu.
Alisema mwili wa mtoto huyo uliokotwa juzi saa 12 jioni na wakazi wa eneo
hilo waliokuwa wakifanya doria tangu alipopotea Februari 15, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Kamanda Konyo, mwili wa marehemu ulikutwa kwenye shamba la
mahindi lililopo katika Hifadhi ya Biharamulo.
“Mwili huo uliokotwa kwa jitihada za wakazi wa Kitongoji cha Mapinduzi,
Kijiji cha Lumasa wilayani Chato waliokuwa doria wakishirikiana na makachero wa
Jeshi la Polisi waliomwagwa huko kwa ajili ya msako wa watu waliohusika na
unyama huo.
“Baada ya mwili huo kuokotwa, ulichukuliwa na kwenda kuhifadhiwa katika Hospitali
ya Wilaya ya Chato, Mkoa wa Kagera ukisubiri uchunguzi na taratibu za mazishi.
GEITA |
“Hata hivyo, hadi sasa tunamshikilia mtu mmoja ambaye hatuwezi kumtaja
jina kwa sababu tunaweza kuingilia upelelezi unaoendelea.
“Tukio hili ni kati ya matukio mabaya sana tena sana, nawaomba Watanzania
wenzangu tujitafakari na kuchunguza matendo yetu ili kuona kama kweli yanampendeza
Mwenyezi Mungu, inaumiza sana kwa kweli,” alisema Kamanda Konyo.
Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Albino Tanzania (TAS),
Mkoa wa Geita, Isaack Timoth, alisema anasikitishwa na vitendo vya ukiukwaji wa
haki za binadamu vinavyofanywa na baadhi ya watu.
Wakati hayo yakitokea,
takwimu zinaonyesha kwamba katika
Wilaya ya Geita, kuanzia mwaka 2007 hadi 2012 albino sita wameshauawa.
Walemavu hao ni Remmy Juma (2), Zakaria Juma (7), wakazi wa Buhalahala, Kata
ya Kalangalala mjini Geita.
Wengine ni Rwegamoyo Kitangili mkazi wa Kijiji cha Chigunga, Zawadi
Magindu (32), mkazi wa Nyamalulu na Gaspa Elikana mkazi wa Nyawilimilwa.
Waliojeruhiwa na kuachwa na vilema vya kudumu kuanzia mwaka 2007 hadi 2011
ni Bibiana Mbushi (9), mkazi wa Nyamwilolelwa aliyekatwa mguu wa kulia na
vidole viwili vya mkono wa kulia na Nelick Elias (4), mkazi wa Kijiji cha
Kaseme aliyenyolewa nywele na watu wasiojulikana.
Wengine ni Adam Robert (12), mkazi wa Nyaruguguna aliyejeruhiwa mkono wa
kushoto na kukatwa vidole vya mkono wa kulia.
Wakati huo
huo, Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini ambaye pia ni Mkurugenzi
Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Alvaro Rodriguez,
amehimiza Serikali ichukue hatua zaidi ili kukabiliana na mauaji ya albino
nchini.Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana baada ya taarifa ya kutekwa na kuuawa kwa Yohana Bahati, Rodriguez alisema pamoja na juhudi zilizopo za kukabiliana na mauaji hayo, kuna kila sababu ya kuongeza nguvu ili kupambana na wahalifu hao.
Taarifa inaeleza pia kwamba, mama wa mtoto huyo, Ester Jonas (30) ambaye alijeruhiwa wakati alipokuwa akiporwa mtoto wake huyo, bado yuko katika Hospitalini ya Rufaa ya Bugando akitibiwa majeraha yaliyosababishwa na mapanga aliyokatwa wakati akigombana na waporaji hao.
Dada yake marehemu, ambaye pia ni albino, Tabu Bahati (3), anaendelea kuhifadhiwa polisi na ndugu yake Shida Bahati (12) anaendelea kulelewa na ndugu zake.
“Katika kipindi cha miezi miwili, Tanzania imeshuhudia kutekwa nyara kwa watoto wawili katika Kanda ya Ziwa.
“Desemba mwaka jana, mtoto Pendo alitekwa na kusababisha kizaazaa kikubwa, lakini pamoja na juhudi za kumtafuta mtoto huyo hadi leo hajulikani alipo,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.-Mtanzania
Maoni
Chapisha Maoni