Yanga yatinga makaburini
KIKOSI cha Yanga kinachonolewa na Mholanzi Hans
van der Pluijm kimehamishia kambi katika Chuo cha Uvuvi Mbegani, Bagamoyo,
ambapo pamoja na mambo mengine, kitatembelea vivutio vya kitalii, yakiwamo makaburi
ya masharifu yaliyopo Kaole, wilayani humo.
Awali Yanga walikuwa wameweka kambi katika Hoteli
ya Kiromo, iliyopo Bagamoyo, kujiandaa na mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara
dhidi ya Polisi Morogoro, uliochezwa Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Jamhuri,
Morogoro ambapo Wanajangwani hao walishinda bao 1-0.
Na kwa sasa timu hiyo ikijiandaa kuivaa Ndanda FC
ya Mtwara Jumapili hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, benchi la ufundi
la Yanga limeona ni vema kujichimbia Mbegani, eneo ambalo ni tulivu
linalowawezesha wachezaji kushika maelekezo ya makocha wao kwa ufanisi wa hali
ya juu.
Lakini pia, kitendo cha wachezaji kutembelea eneo
la Kaole kujionea vivutio vya kitalii vya huko, yakiwamo makaburi ya masharifu,
ni njia mojawapo ya kuwajenga kisaikolojia.
Wakiwa katika makaburi hayo ya Kaole, wachezaji
hao watapata fursa ya kuliona kaburi la Wapendanao waliozikwa pamoja na lile la
Sharifu ambalo hutumika kwa ajili ya kuomba dua kupata baraka kuelekea michezo
yao ijayo.
Bagamoyo ni miongoni mwa miji maarufu ya kihistoria
ambapo enzi za utumwa, wafanyabiashara wa Kiarabu na kizungu waliutumia
kupitisha biashara zao.
Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema kuwa sababu
ya kambi kuhamishiwa Mbegani kutoka Kiromo Hotel, pamoja na mambo mengine ni
kukwepa hujuma zozote zinazoweza kufanywa na wapinzani wao kupitia nyota wao.
Chanzo kutoka ndani ya kambi hiyo kimesema kuwa benchi la ufundi limeona Mbegani ni eneo salama na tulivu zaidi kwa
wachezaji wao kujifunza mambo mbalimbali kutoka kwa makocha wao.
“Unajua kwa sasa inaonekana hakuna timu
inayopenda kuona mpinzani wake anashinda, hivyo tumeona ni vema tukaweka kambi
Mbegani na kutembelea eneo la Kaole kama sehemu ya kuwajenga zaidi wachezaji
wetu kuelekea mechi zetu zijazo,” alisema mtoa habari huyo.
Akizungumza na BINGWA, Meneja wa Yanga, Afidh
Saleh, alikiri timu yao kukimbilia Mbegani, lakini pia akiweka wazi juu ya wazo
la kutembelea eneo la Kaole ili kutoa fursa kwa wachezaji kujionea mambo
mbalimbali ya kihistoria.
“Ni wazo zuri (kwenda kutembelea vivutio vya
kitalii vya Kaole), ...tutakwenda huko bila shaka,” alisema Saleh.
Mbali ya mechi za Ligi Kuu Bara, Yanga pia
inakabiliwa na kibarua cha michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, ikiwa
imepangwa kuanza na BDF XI ya Botswana ambapo mchezo wa kwanza utapigwa kati ya
Februari 13 na 15, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kutokana na kukabiliwa na michezo hiyo ya ligi na
ya kimataifa, Yanga wamekuwa wakijinoa vilivyo kuhakikisha wanafanya vizuri.
Jana kikosi hicho kilifanya mazoezi kwenye Uwanja
wa Chuo cha Uvuvi Mbegani tayari kabisa kuwavaa Ndanda FC, huku wachezaji wote
wakiwa na ari kubwa ya kuibuka na ushindi.
Baada ya mchezo huo wa Jumapili, Yanga watashuka
tena dimbani Jumatano ijayo kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kuivaa Coastal
Union ya huko.-bingwa
Maoni
Chapisha Maoni