Simba wataka mkutano mkuu
WANACHAMA wa Simba kutoka matawi mbalimbali nchini, wameujia
juu uongozi wao na kutaka kuitishwa kwa mkutano mkuu ili kujadili mambo
mbalimbali yanayowakabili kwa sasa, ikiwa ni pamoja na mwenendo usioridhisha wa
timu yao katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Wanachama hao waliowakilishwa nakatibu msaidizi wa
matawi ya Simba, Wilaya ya Temeke, Ally Bane, alisema anahitaji mkutano wa
dharura ili waweze kujadili mustakabali wa timu, kwani kunaonekana kuwapo kwa mpasuko
ndani ya viongozi wa klabu hiyo.
Alisema kama mkutano huo hautafanyika, watasusia
kwenda uwanjani kutokana na mwenendo wa matokeo mabaya ya timu hiyo.
“Mkutano ndio utakuwa suluhisho, la sivyo hatuna
haja ya kwenda uwanjani na matokeo haya ambayo kikosi chetu yanapata, tumechoka
kila siku sisi tu,”alisema.
Naye Mwenyekiti wa matawi ya Simba Mkoa wa Tanga,
Mbwana Msumari, alimtaka Rais wa timu hiyo, Evans Aveva kurudisha umoja kwenye klabu hiyo.
“Hapa umoja ukirudi timu itaweza kufanya vema la
sivyo msimu huu tutashuka daraja tusipoangalia, Aveva anatakiwa
atuokoe,”alisema.
BINGWA lilimtafuta Katibu Mkuu wa timu hiyo,
Stephano Ali,ambaye alisema wanapambana kuweka mambo sawa.-bingwa
Maoni
Chapisha Maoni