Ndemla ahusishwa kipigo Simba
KOCHA Mkuu wa Simba, Mserbia Goran Kopunovic,
amekiri kuwa kukosekana kwa kiungo wake Said Ndemla na mshambuliaji Emmanuel
Okwi kumechangia timu yake kufungwa mabao 2-1 na Mbeya City katika mchezo wa
Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ndemla aliukosa mchezo huo kutokana na kuumia
nyama za paja, wakati Okwi akiwa ni majeruhi baada ya kugongwa kichwani na beki
wa Azam, Aggrey Morris na kupoteza fahamu katika mechi baina ya timu hizo
iliyopigwa mwishoni mwa wiki iliyopita.
Akizungumza baada ya mechi ya juzi, Goran alisema
katika kikosi chake kulikuwa na pengo kubwa kwa kukosekana wachezaji hao na
kwamba anapokuwa Ndemla katika kikosi chake, anakuwa na msaada mkubwa hasa kwenye
kusaidia mashambulizi.
Alisema kuwa alilazimika kumtoa Danny Sserunkuma
na nafasi yake kuchukuliwa na Elius Maguli kwa kuwa Mganda huyo alionekana kuchoka
kwa kile alichodai kucheza mechi nyingi mfululizo kuanzia michuano ya Kombe la
Mapinduzi Zanzibar hadi ya Ligi Kuu Bara.
Goran alisema tatizo lingine ambalo huwa
linagharimu timu hiyo na hali nzima ya wachezaji wake kutokuwa na pumzi za kutosha
na hivyo kushindwa kuhimili dakika zote 90.
“Kikosi kimekosa uimara, hasa kwa wachezaji
kuonekana kuchoka mapema kabla ya dakika 90, lakini pia kukosekana kwa Okwi na
Ndemla kuliigharimu timu kwani mara kadhaa akiwepo Ndemla huwa anasaidia sana
kupeleka mashambulizi mbele,” alisema.
Tayari Ndemla na Okwi wameanza mazoezi mepesi na
iwapo hali zao zitaimarika, huenda wakajumuika na wenzao katika mechi zijazo
japo uwezekano wa kucheza kesho dhidi ya JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa ni
mdogo-Bingwa
Maoni
Chapisha Maoni