Majambazi yatikisa Zanzibar
MAJAMBAZI yametikisa viunga vya Mtaa wa Darajani kisiwani
Zanzibar na kusimamisha shughuli za biashara wakati polisi walipowakimbiza na
kuamua kutumia risasi za moto.
Tukio hilo lilitokea jana saa nane mchana na kusababisha
watu wawili kujeruhiwa na watatu kupoteza fahamu kutokana na vishindo vya risasi
na mabomu wakati majambazi hayo yalipotaka kutoroka.
Taarifa zaidi zinasema gari ya majambazi hayo iliwagonga wanawake
wawili baada ya kuingia kwa kasi katika eneo la wafanyabiashara wa Darajani
maarufu kwa jina la Jua Kali.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo walisema majambazi hayo yalikuwa
na gari aina ya Toyota Noah yalikimbizana na polisi na walipofika katika kituo
cha zamani cha daladala walipotea njia kwa kutaka kupita kulia kabla ya gari
yao haijakwama katika ukuta wa Shule ya Msingi Darajani.
Mkazi wa Michenzani, Said Musa Ali, alisema wakati wakishangaa
gari hiyo kuingia kwa kasi, ghafla wanawake wawili waligongwa na kusukumwa pembeni
huku wengine wakipiga kelele baada ya milio ya risasi kutokea.
Alisema ndani ya gari hiyo kulikuwa na dereva na abiria watatu
na waliteremka wakiwa na silaha wakataka kukimbia.
Naye, Halima Mohamed, alisema akiwa amejificha chini ya
meza aliona moja kati ya majambazi hayo akipigwa risasi kichwani na kudondoka
chini huku mwezake akizungukwa na wananchi waliokuwa na hasira.
Alisema dereva wa gari hiyo alitoka upande wa kushoto na
kufanikiwa kuruka ukuta wa shule hiyo wakati tayari wananchi wakimkimbiza.
“Kama si mlipuko wa risasi, wananchi walimkamata dereva
yule mguu wakati anaruka ukuta lakini kwa bahati mbaya wakati wanamshika
kulitokea kishindo cha risasi wakamwacha baada ya kukumbwa na hofu,” alisema
Omar Suleiman.
Baadhi ya wafanyabiashara wadogo katika eneo hilo walitupa vifaa
vya kufanyia biashara zao baada ya kutokea milio ya risasi.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi,
Mkadam Khamis Mkadam, alisema majambazi hayo yalikuwa yamegawanyika makundi
mawili huku wengine yakifanikiwa kukimbilia katika eneo la Fumba lililopo nje
ya mji.
Alisema operesheni ya kuwasaka majambazi hayo na dereva
aliyekimbia inaendelea kufanyika kwa ustadi mkubwa.
“Tukio hilo lilitokea saa nane mchana na kusababisha biashara
kusimama kwa muda katika eneo hilo huku watu wakikimbia ovyo baada ya askari wa
kikosi cha kupambana na ujambazi kuanza kurusha risasi wakati wakitafuta njia
ya kuwakamta majambazi hayo yakiwa salama.
“Wafanyabiashara wa Soko la Darajani walioshuhudia tukio
hilo walisema kwamba ulikuwa kama mchezo wa kuigiza wakati askari hao
wakikimbizana na majambazi hayo na kusababisha njia kuu ya Darajani kufungwa
kwa muda baada ya majambazi kupotea njia na kuingia katika barabara isiyopitisha
magari.
“Hali ilikuwa mbaya kila mtu alishindwa kuamini baada ya
kuanza kusikia milio ya risasi watu wakikimbia ovyo, jambo la kushukuru
wananchi walifanya ujasiri mkubwa kwa kushirikiana na polisi hadi kuwakamata
wakiwa na silaha zao,” alisema Mkadam.
Katika hatua nyingine, Mganga wa zamu wa Hospitali ya Rufaa
ya Mnazi Mmoja Zanzibar, Dk. Marijani Msafiri, alisema watu watano walifikishwa
hospitalini hapo wakiwemo majeruhi wawili wanaoendelea na matibabu.
Alisema kati ya hao, wengine walikuwa wakisumbuliwa na
tatizo la kutojitambua kutokana na mshituko na kukumbwa na hofu lakini
waliendelea kutibiwa.-Mtanzania
Maoni
Chapisha Maoni