Maiti zakutwa zikielea juu ya maji
WATU wawili mkoani Singida, wamefariki dunia katika matukio
mawili tofauti katika wilaya za Iramba na Singida na miili yao kukutwa ikielea
juu ya maji.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Simon Haule, amesema
tukio la kwanza lilitokea Januari 26, mwaka huu, saa 2.30 asubuhi katika
ziwa dogo la Singidani mjini Singida, ambapo mwili wa mwanamke anayekadiriwa
kuwa na umri kati ya miaka 60 na 65 ambaye hakufahamika jina wala makazi yake,
uliokotwa na wavuvi ukiwa unaelea juu ya maji.
Amesema maiti ya marehemu huyo imehifadhiwa katika chumba
cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mkoa wa Singida.
Kamanda huyo, ametoa wito kwa ndugu na jamaa waliopotelewa
na ndugu yao wa jinsia ya kike wafike hospitalini hapo kuutambua mwili
huo.
Katika tukio jingine, Kamanda Haule, ameongeza kuwa siku hiyo hiyo,
saa 5 asubuhi, katika Kijiji cha Nsunsu, Kata ya Ntwike, Tarafa ya Shelui
wilayani Iramba, mwili wa mtoto Emmanuel Amosi (5) umeokotwa ukiwa unaelea
kwenye maji ya bwawa linalotumika kunyweshea mifugo.
"Uchuguzi wa awali unaonyesha kuwa mtoto huyo alikuwa
anaogelea, na ndipo akazidiwa na maji na hatimaye kupoteza maisha," Kamanda Haule.
Kutokana na hali hiyo, Kamanda Haule ametoa wito kwa
wananchi mkoani hapa kuchukua tahadhari na mvua zinazoendelea kunyesha hivi
sasa na hasa wakati wa kuvuka mito inayofurika maji.
Maoni
Chapisha Maoni