Bibi kizee aanguka kwenye ndege yake akiwa anasafiri
Akutwa uchi, wananchi wataharuki, polisi yamwokoa
KATIKA hali ya kushangaza, bibi kizee anayekadiriwa
kuwa na umri wa miaka (70), asiyejulikana jina wala makazi yake, ameanguka
akiwa uchi wa mnyama nyumbani kwa Suzana Mwandu, mkazi wa Mtaa wa Mageuzi
mkoani Shinyanga.
Tukio hilo lilitokea juzi ambapo bibi huyo baada ya
kuanguka alianza kutembelea makalio bila kuzungumza chochote jambo ambalo
limedaiwa ni ushirikina.
Bibi anayedhaniwa kuwa mchawi akiwa amelala juu ya mawe
baada ya kutoa pesa alizokuwa nazo kiuoni na kuwatupia wananchi wa mtaa wa
Mageuzi.
|
Akielezea tukio hilo jana, Mwandu alisema lilitokea nje ya nyumba ambapo
alishangazwa kumkuta kikongwe huyo akiwa amelala huku akiwa uchi wa mnyama.
Mwandu alisema baada ya kikongwe huyo kuanguka,
alijivuta hadi kwenye jiko lake lililoko nje ya nyumba ambalo lipo wazina baada
ya kuanza kumsemesha ndipo akazinduka na kuanza kuongea maneno yasiyoeleweka,
hali ambayo ilimtia wasiwasi na kutoa taarifa kwa uongozi wa Serikali ya Mtaa.
“Nyumba yangu nimeizindika vilivyo, hivyo kikongwe
huyu alipokuwa katika safari zake na kupita maeneo ya nyumbani kwangu ndipo
akakutana na balaa hilo na hatimaye akajikuta ameanguka na kuingia jikoni kwa
ajili ya kujificha.
“Unajua siku zote mchawi anapoanguka na ukimwacha kwa muda mrefu bila ya
kumsemesha, anaweza kupoteza maisha, hivyo kutokana na mimi kutokuwa na ubaya
naye, nikaona bora nimsemeshe ili kumwokoa na baada ya hapo nikampa nguo za
kujistiri na aibu ya kuwa mtupu,” alisema Mwandu.
Kwa upande wao mashuhuda wa tukio hilo, walidai kuwa
bibi huyo huenda akawa ni mchawi kutokana na kauli zake tatanishi alizokuwa
akizitoa huku mikono yake ikionekana kukatwa kwa mapanga na kuota sugu.
“Huyu bibi atakuwa mchawi, angalia hata mikono yake
imekatwa katwa na imekomaa kweli, huenda huwa anajigeuza fisi na kutembelea
mikono, halafu macho yake siyo ya kawaida, ana kiburi kupita kiasi na ndiyo
tabia za wachawi wengi,”alieleza Halima Juma.
Hata hivyo, bibi huyo alifanya kituko kwa kuanza
kutoa frdha za noti na sarafu alizokuwa amezihifadhi kiunoni kwa kutumia
kitambaa cheusi huku akizirusha juu na katika hali ya kushangaza alipata nguvu
na kuinuka.
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mageuzi, Waziri Mussa
(Chadema), alikiri kuwepo kwa tukio hilo
ambalo lilijaza umati wa watu, huku wakishindwa kumtambua kikongwe huyo
alikotokea na alikokuwa akielekea.
Alisema wakati wakiendelea kumuhoji na kumpa uji, alipata fahamu na wakati huo
huo polisi walikuwa wamekwishafika na hivyo kumnusuru bibi huyo kushambuliwa na
wananchi waliokuwa na hasira.
Hata hivyo, askari hao walishindwa kwenda naye
kituoni kwa kile walichodai kwamba Serikali haiamini uchawi na kumruhusu bibi
huyo kuendelea na safari yake.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Longunus
Tibishubwamu, alithibitisha kutokea tukio hilo.-Mtanzania
Maoni
Chapisha Maoni