Wauaji wa Ubungo wahukumiwa kunyongwa, Ni wale waliohusishwa na uporaji wa fedha za NMB
Mahakama
Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetoa hukumu ya kunyongwa hadi kufa kwa washtakiwa sita
katika kesi ya mauaji ya askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wa
mkoani Morogoro na mfanyakazi wa Benki ya NMB, maarufu kama mauaji ya Ubungo
Mataa.
Washtakiwa
hao waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa jana na Jaji Projest Rugazia ni Haji
Kiweru, Mashaka Pastory, Wycliff Imbora, John Mndasha, Martine Mndasha na
Rashidi Abdikadir.
Jaji
Rugazia alidai kwamba aliwatia hatiani washtakiwa hao na kuwahukumu kunyongwa
hadi kufa kutokana na ushahidi ulitolewa na mashahidi 29 upande wa mashtaka
pamoja na vielelezo 78 vilivyowasilishwa mahakamani hapo na ushahidi wa
utetezi.
“Maungamo
ya washtakiwa, ushahidi wa kitaalam na utambuzi wa washtakiwa kutambiliwa eneo
la tukio inaonesha wazi kwamba walikuwa na nia ya kujaribu kupora takribani Sh milioni
150 ambazo ni mali ya benki ya NMB zilizokuwa zikisafirishwa kutoka Dar
es Salaam kwenda Morogoro tawi la Wami,” Alidai Jaji Rugazia.
Alidai
siku hiyo ya huzuni ya Aprili 20 mwaka 2006, majambazi hao
walilivamia gari hilo kwa lengo la kupora lakini bila ya huruma yoyote
walilimiminia risasi na kumwua askari huyo mwenye namba D 6866, Konstebo
Abdallah Marwa na mfanyakazi wa NMB tawi la Wami Morogoro, Ernest Manyonyi.
Alidai
washtakiwa walifanya tukio hilo katika eneo la Ubungo mataa jijini Dar es
Salaam saa 6:30 mchana katika makutano ya barabara ya Morogoro na Sam Nujoma.
Hata
hivyo Jaji Rugazia aliwaachia huru washtakiwa Rashid Lemblisi, Philipo Mushi, Yassin Juma,Hamisi Daud, MT 77754 Nazareth Amurike, MT 76162 Emmanuel
Lameck, James
Chamangwana na Hussein Idd baada ya kukutwa hawana hatia katika kesi hiyo.
Kwa
upande wa washtakiwa, Jackson Issawangu aliyekuwa mshtakiwa wa sita katika kesi
hiyo na Mussa Mustafa aliyekuwa mshtakiwa wa 10 waliachiwa huru awali baada ya
mahakama hiyo kuwaona kuwa hawana kesi ya kujibu.
Hadi
wanaachiwa huru hapo jana washtakiwa hao walikuwa wamekaa rumande kwa
muda wa zaidi ya miaka 8.
Awali
wakati kesi hiyo ilipokuwa ikisikilizwa, mahakama hiyo ilitupilia mbali
vielelezo muhimu vya ushahidi katika kesi hiyo ya mauaji ikiwemo ripoti
saba, kati ya nane za uchunguzi wa silaha zilizotumika katika mauaji hayo.
Hatua
hiyo ilichukuliwa baada ya Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Godfrey
Luhamba, Mtaalam wa milipuko kuiomba mahakama hiyo ipokee ripoti hizo
kama vielelezo vya ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo.
Mawakili
wa upande wa utetezi wakiongozwa na Richard Rweyongeza, walipinga ripoti hizo
kupokewa, wakidai kuwa ziliwasilishwa kinyume cha sheria kwa kuwa hazikusomwa
kwa washtakiwa wakati wa kuhamisha kesi hiyo kutoka Mahakama ya Kisutu kwenda
Mahakama Kuu.
Katika
uamuzi wake, Jaji Rugazia alikubaliana na utetezi kuwa kwa kuwa ripoti
hizo hazikuwahi kusomwa kwa washtakiwa, basi mahakama hiyo haiwezi kuzipokea
kwa sababu ziliwasilishwa kinyume cha sheria.
Pia
alikataa hoja za upande wa mashtaka kutaka mahakama iamuru washtakiwa hao
warudishwe tena mahakama ya chini (Kisutu), wakasomewe ripoti hizo, au iamuru
upande wa mashtaka uwapatia upande wa utetezi wapate muda wa kuzipitia na kisha
kuendelea.
Alidai
mapendekezo hayo ya upande wa mashtaka hayaungwi mkono na kifungu chochote cha
sheria.
Hata
hivyo mahakama hiyo ilipokea ripoti moja tu ambayo ndio iliyosomwa kwa
washtakiwa katika mahakama ya chini, ambayo inabainisha kuwa maganda mawili ya
risasi, yaliyopatikana katika eneo ya tukio yalitoka kwenye bastola mojawapo zilizokamatwa
kwa washtakiwa.
Ripoti
nyingine zilizokataliwa ni zile zinazohusu bastola nane, SMG tano na Shortgun
moja ambazo zote zilikamatwa kwa washtakiwa.-Mtanzania
Maoni
Chapisha Maoni