Wanafunzi watumikishwa kupata fedha za chaki
WANAFUNZI
wa Shule ya Msingi Karukekere katika Wilaya ya Bunda wamefanyishwa kazi za vibarua mashambani
na walimu ili kupata fedha za kununulia chaki kitendo ambacho kilichopingwa
vikali na wananchi.
Tukio
hilo liliwasilishwa kwenye mkutano wa
hadhara ulioitishwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), Boniphace
Mwita pamoja na Mwenyekiti wa CCM wilayani Bunda, Chacha Gimanwa.
Wakitoa
malalamiko yao, wananchi hao walisema wanafunzi wamekuwa wakitumia muda mwingi kufanya kazi za
vibarua zikiwamo za kulima mashamba ya watu binafsi wakati wa vipindi vya
masomo ikiwa ni pamoja na kutembea umbali mrefu kwenda kwenye mashamba hayo.
Walisema
baada ya kuona watoto wakiwa mashambani, walikwenda kuwahoji walimu
kuhusu hali hiyo na walijibiwa kwamba wanafanya hivyo zipatikane fedha za kununua chaki na mahitaji
mengine ya shule hiyo.
Aidha,
walisema kuwa hali hiyo imekuwa ikisababisha wanafunzi kutopata muda wa kusoma
hali ambayo pia inachangia kushuka kwa kiwango cha elimu shuleni hapo, kwani
watoto wamekuwa hawafanyi vizuri katika masomo yao.
"Watoto
wetu wanafanyishwa kazi za vibarua vya kulima tena wanatembea umbali mrefu
sana, wakati wa masomo sasa walimu hawa wanasababisha kiwango cha elimu kushuka
katika shule hiyo" alisema mzazi mmoja.
Akijibu
kero za wananchi hao, Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Bunda, Gimanwa alisema kuwa
ni kosa kubwa walimu hao kutumikisha wanafunzi katika vibarua badala ya
kuwafundisha.
Gimanwa
alisema kuwa kuwapo kwa hali hiyo shuleni hapo kunasababishwa na uongozi wa
serikali ya kijiji hicho pamoja na kamati ya shule hiyo kutokuwa imara kufuatilia
malalamiko ya wananchi hao na kuzuia hali hiyo.
Alisema
kuwa fedha za kuendesha shule za msingi na sekondari zimekuwa zikitolewa na
serikali mara kwa mara na kwamba kwa hali hiyo hakuna haja ya kutumikisha
wanafunzi kufanya vibarua kwa kisingizio cha kupata fedha za
kununulia chaki na mahitaji mengine.
Kutokana
na tukio, viongozi hao waliahidi kulifikisha kwa afisa elimu shule za
msingi katika wilaya hiyo.
Maoni
Chapisha Maoni