Umeisikia hii ya Bomu kumuua aliyetaka kuua polisi Songea
MTU mmoja amefariki dunia papo hapo baada ya bomu
alilotaka kuwarushia askari waliokuwa doria ya Sikukuu ya Krismasi katika Mtaa
wa Kotazi uliopo Kata ya Majengo, Manispaa ya Songea, kumlipukia.
Kutokana na tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia
jana, Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma kwa kushirikiana na makachero kutoka makao
makuu ya jeshi hilo yaliyopo Dar es Salaam, wanawasaka watu watatu walioshirikiana
na mlipuaji huyo ambaye bomu hilo lilimshinda na kumlipukia huku utumbo wake ukitoka
nje na mkono wake wa kushoto umekatika na
vipande vyake havijulikani vilipo.
Akizungumza mjini hapa jana katika ukumbi wa
mikutano wa jeshi hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athumani,
alisema tukio hilo lilitokea saa saba usiku wakati askari wakiwa doria.
Alisema wakati doria inaendelea katika eneo hilo, kulitokea
mlipuko wa bomu lililotengenezwa kienyeji na kuwajeruhi askari wawili.
Aliwataja askari waliojeruhiwa kuwa ni PC Mselemu
mwenye namba G 7903, ambaye alijeruhiwa mkono wake wa kushoto na alitibiwa na
kuruhusiwa na mwingine ni PC Mariam mwenye namba WP. 8616, naye alijeruhiwa
bega la mkono wa kushoto na amelazwa katika Hospitali ya Mkoa Ruvuma akiendelea
kupata matibabu.
Alisema timu ya makachero watahakikisha watuhumiwa watatu
waliohusika na tukio hilo wanakamtwa kwa kufuatilia mtandao wao wa uhalifu, kwa
kuwa vitendo vya ulipuaji wa mabomu vimekithiri nchini, ikiwemo Ruvuma kwa kuwa
hadi sasa ni tukio la tatu kwa mwaka huu.
Alisema wahalifu hao watakamatwa kutokana na tukio hilo
kwa sababu baada ya mwenzao kulipuliwa na bomu hilo, walijaribu kutorosha mwili
wake ili kupoteza ushahidi lakini ilishindikana baada ya askari wengine
waliokuwa doria kuwahi eneo la tukio na wao wakaamua kukimbia kusikojulikana.
“Wahalifu hao waliuvuta mwili wa mwenzao kutoka
katika eneo la tukio kwa umbali wa mita zisizopungua 80 na 90 kwa lengo la
kutaka kupoteza ushahidi, lakini waliwahiwa na askari wengine wa doria na
kuuacha mwili na kutokomea kusikojulikana,” alisema Athumani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said
Mwambungu, aliyetembelea eneo la tukio alisema wahalifu hao wanaishi katika
jamii inayotuzunguka, hivyo ni vyema kila mmoja akaliona tukio hilo kwa umuhimu
wake na kuwafichua waliofanya ili Ruvuma iendelee kuwa na amani kwa kuwa inaleta
taharuki na kurudisha nyuma shughuli za maendeleo.
Naye, Mganga Mkuu Mfawidhi Hospitali ya Mkoa wa
Ruvuma, Dk. Benedkto Ngaiza, amethibitisha kupokea mwili mmoja wa mtu aliyefariki
huku utumbo ukiwa umetoka nje na majeruhi wawili ambao ni askari.-Mtanzanuia limeripoti
Maoni
Chapisha Maoni