Mwanamke achoma moto nyumba ya mumewe
MKAZI wa Kijiji cha Majengo, Kata ya
Koryo Wilaya ya Rorya Mkoa wa Mara, Vaileth Ogola, anatafutwa na polisi kwa
tuhuma za kuhusika na tukio la kuchoma nyumba ya mumewe moto na kuteketeza mali
zilizokuwamo.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa
Polisi Mkoa wa kipolisi wa Tarime na Rorya, Lazaro Mambosasa, alisema kuwa
tukio hilo lilitokea Desemba 23 mwaka huu saa mbili usiku mara baada ya kutokea
ugomvi baina yake na mumewe.
“Tukio hili linadaiwa kuwa chanzo
chake ni ugomvi uliosabaishwa na wivu wa kimapenzi baina ya mtuhumiwa na mumewe,
Kinyatta Kibindi, lakini baada ya kufanikiwa kuichoma moto nyumba hiyo
alitoroka na kwenda ambako hakujajulikana na hivyo Jeshi la Polisi linamsaka,” alisema.
Hata hivyo, Kamanda alisema kuwa mumewe
Kibindi ni mkazi wa Dar es Salaam na alikuwa ameenda kijijini hapo kwa nia ya
kusherehekea sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya lakini sasa hana makazi ya
kuishi yeye pamoja na wapangaji saba waliokuwa wakiishi katika nyumba hiyo.
“Thamani ya mali iliyoteketea ndani
ya nyumba hiyo ikiwa ni pamoja na zile za wapangaji saba bado haijajulikana
hadi sasa, mtuhumiwa akikamatwa atafikishwa mahakamani kwa ajili ya kujibu
tuhuma zinazomkabili,” alisema.
Maoni
Chapisha Maoni