Mke amrudisha Okwi Uganda
BAADA ya kuiwezesha Simba kuitungua Yanga mabao 2-0
katika pambano la Nani Mtani Jembe, straika Emmanuel Okwi leo Jumanne anaondoka
nchini kwenda Uganda kwaajili ya kusherehekea harusi yake.
Okwi alifunga ndoa ya kimila hivi karibuni akiwa mapumzikoni
nchini kwao Uganda, hatua iliyopelekea kuchelewa kujiunga na kikosi cha Simba
kilichokuwa kinajiandaa na mechi ya Nani Mtani Jembe dhidi ya Yanga.
Straika huyo alikuwa sehemu ya kikosi cha Simba kilichoibuka
na ushindi dhidi ya Yanga katika pambano la Nani Mtani Jembe lililopigwa
Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mabao ya Simba katika mchezo huo yalizamishwa wavuni
na Awadh Juma na Elias Maguli.
Akizungumza jana, Okwi alisema baada ya
sherehe ya harusi iliyohusisha upande wa ndugu zake, leo anarejea nchini kwake katika
tafrija nyingine itakayofanyika upande wa laazizi wake.
“Unajua ndoa niliyofunga hivi karibuni ilihusisha
upande wa familia yetu kwa hiyo narudi Uganda kwaajili ya sherehe ya
utambulisho itakayofanyika Desemba 20 upande wa mke wangu.
“Baada ya kusherehekea harusi ya kimila katika
familia zote mbili, Julai mwakani ndiyo natarajia kufunga ndoa ya kanisani,” alisema
Okwi.
“Wanasimba wasiwe na hofu kwani nitarejea haraka
kujiunga na wenzangu kwa ajili ya
maandalizi ya ligi kuu kama unavyojua tumepania kufanya vizuri msimu huu.”-Hisani ya Bingwa
Maoni
Chapisha Maoni