Mgombea wa Chadema, kampeni meneja wauawa
ALIYEKUWA mgombea nafasi ya
uenyekiti wa Kitongoji cha Idodomya Kata ya Kanoge Wilaya ya Kaliua mkoani
Tabora, Williamu Masanilo (Chadema) na mpambe wake Juma Ujege, wameuawa kwa
kukatwa kichwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora,
Suzan Kaganda alisema tukio hilo ni sawa na matukio mengine ya ujambazi na
kukanusha taarifa zilizodaiwa kuwa lina uhusiano na masuala ya kisiasa.
Alisema tukio hilo limetokea Desemba
24 mwaka huu saa 8 usiku ambapo watu wasiojulikana walivamia nyumbani kwa
William Masanilo ambaye ni mfanyabiashara na kufanikiwa kumchoma na kitu chenye
ncha kali kichwani na hivyo kumsababishia kifo chake.
“Wavamiaji hao walitaka fedha, baada
ya kumuua walimgeukia mfanyakazi wake ambaye walitaka atoe fedha lakini
alipowajibu hajui walimpiga na kitu kizito kilichosababisha kupasuka kichwani
na hivyo kufariki, uchunguzi wetu awali wa unaonyesha hili tukio ni la ujambazi
na si la siasa,” alisema kamanda.
Katibu wa Chadema Wilaya ya Kaliua,
Rajabu Hamisi yeye alisema tukio hilo lilipangwa kwa lengo la kumwondoa mgombea
wao na ndiyo maana limetekelezwa siku chache kabla ya kurudia uchaguzi wa
marudio wa Serikali za Mitaa.
“Iwapo ni tukio la ujambazi
asingeuawa mgombea wetu na kampeni meneja wake kipindi ambacho tunasubiria
kurudia uchaguzi utakaofanyika Desemba 27, mwaka huu,” .-Chanzo Mtanzania
Maoni
Chapisha Maoni